• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
TAHARIRI: Serikali ieleze iwapo kuna ongezeko la maambukizi ya Covid-19

TAHARIRI: Serikali ieleze iwapo kuna ongezeko la maambukizi ya Covid-19

NA MHARIRI

KWA wiki chache sasa, kumekuwa na wasiwasi katika baadhi ya sehemu za nchi kuhusu homa ambayo inaonekana kuenea kwa kasi.

Baadhi ya wataalamu tayari wameshajitokeza na kueleza hofu kwamba, huenda kuna wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona.

Hofu hii imetiliwa mkazo na jinsi idadi ya watu wanaopatikana kuambukizwa Covid-19 imekuwa ikiongezeka kwa siku chache zilizopita.

Licha ya haya, hatujaona maafisa wakuu serikalini hasa kutoka kwa Wizara ya Afya wakieleza wananchi kuhusu kinachoendelea, na kusisitiza tahadhari zozote za kipekee zinazohitaji kuchukuliwa.

Wananchi wengi hasa katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakifichua jinsi wanavyokumbwa na maradhi ambayo yanaashiria dalili za Covid-19.

Tunapoelekea katika msimu wa sherehe za Desemba, itakuwa ni muhimu kuwe na mwelekeo mahususi ili kuepusha msambao wa homa hii zaidi kwa njia inayoweza kuletea nchi hasara.

Ni muhimu wananchi wajulishwe na asasi husika za serikali kuhusu kama ni kweli kuwa kuna wimbi jipya la maambukizi, na kama kuna sababu zozote za umma kuwa na wasiwasi kuhusu wimbi hilo.

Hakutakuwa na manufaa yoyote kuendelea kuwaacha raia kuishi kwa kubahatisha kuhusu kama maisha yao yako salama wanapoendelea na shughuli zao za kawaida.

Kuna shughuli nyingi ambazo zinatarajiwa kufanywa na wengi mwezi ujao wa Desemba katika pembe zote za nchi.Baadhi ya shughuli hizo, ikiwemo za utalii huwa zinategemea safari za hapa na pale.

Lakini kama ilivyoshuhudiwa katika miaka iliyopita, hofu inaweza kuathiri vibaya biashara za wawekezaji wa sekta tofauti ambao wanatarajia kuzoa faida msimu wa likizo. Ikumbukwe kuwa, biashara hizi zinapopata hasara itakuwa pia ni hasara kwa kapu la ushuru wa taifa.

Vilevile, wananchi wanaotaka kutangamana na wenzao wakati wa likizo wanahitaji kuwa na utulivu wa kiakili watakapofanya hivyo.

Si haki kwa kuendelea kukaa gizani kuhusu kama homa inayoenea ni hatari kwa maisha yao ilhali serikali ina wajibu wa kuwaarifu kuhusu kinachoendelea.

Kuwajulisha wananchi kuhusu homa hii pia ni muhimu ili waweze kujua hatua wanazofaa kuchukua kujilinda wenyewe pamoja na wapendwa wao na wananchi wengine.

You can share this post!

Tungali imara, maseneta wa Azimio wasema

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Mteremko kwa Ubelgiji na Brazil,...

T L