• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 4:21 PM
TAHARIRI: Serikali ifichue mashirika yaliyopigwa marufuku kupeleka Wakenya ughaibuni kusaka ajira

TAHARIRI: Serikali ifichue mashirika yaliyopigwa marufuku kupeleka Wakenya ughaibuni kusaka ajira

NA MHARIRI

HATUA ya serikali kupokonya leseni mashirika 26 ambayo yamekuwa yakisafirisha Wakenya ughaibuni kwenda kusaka ajira, ni habari njema.

Hatua hiyo ni ithibati kwamba serikali haijafumbia macho masaibu ambayo maelfu ya Wakenya wamekuwa wakipitia mikononi mwa waajiri wao katika mataifa ya Uarabuni na nchi nyinginezo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Leba Florence Bore, mashirika hayo 26 yalipokonywa leseni baada ya serikali kufanya uchunguzi dhidi ya kampuni 700 ambazo zimekuwa zikisafirisha Wakenya ughaibuni kutafuta ajira, zikiwemo kazi za nyumbani.

Bi Bore amefichua kuwa baadhi ya kampuni zilizopigwa marufuku zimekuwa zikikiuka sheria na kujihusisha katika ulanguzi wa binadamu.

Baadhi ya kampuni hizo pia zinatumika katika ulanguzi wa dawa za kulevya.

Inawezekana idadi kubwa ya Wakenya ambao wamekuwa wakiteseka katika nchi za Uarabuni walisafirishwa na haya mashirika yasiyojali sheria wala haki za kibinadamu.

Inaaminika kuwa Wakenya zaidi ya 100,000 wanafanya kazi za nyumbani katika mataifa ya Uarabuni.

Visa vya Wakenya kurejeshwa humu nchini kwenye majeneza baada ya kuuawa kwa mateso na waajiri wao vimekuwa vikiongezeka kila uchao.

Takwimu zinaonyesha kuwa Wakenya zaidi ya 90 waliuawa wakifanya kazi za nyumbani Uarabuni kati ya 2019 na 2021. Wengi wao walipoteza maisha yao nchini Saudi Arabia – ambayo ni nchi ya tatu ambapo Wakenya wanatuma kiasi kikubwa zaidi cha fedha nyumbani Kenya.

Kupokonya leseni mashirika hayo hakutoshi. Wamiliki wa mashirika ambayo yamekuwa yakikiuka sheria kwa kujihusisha katika biashara haramu ya ulanguzi wa binadamu na dawa za kulevya, wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Serikali haina budi kuweka wazi orodha ya mashirika yaliyopokonywa leseni. Wamiliki wa mashirika hayo pia waanikwe peupe. Hatua hiyo itasaidia kuhakikisha kuwa Wakenya hawahadaiwi na mashirika hayo.

Kumekuwa na visa kadhaa nchini ambapo matapeli wanaibia Wakenya wanaosaka kazi hela zao kwa kuwahadaa kwamba watawasaidia kupata ajira ughaibuni na kisha kutoweka.

Idadi kubwa ya mashirika ya kusafirisha Wakenya ughaibuni kusaka ajira yanamilikiwa na wanasiasa au watu walio na ushawishi serikalini. Hivyo, kuna hofu kwamba huenda mchakato huo wa kukabiliana na mashirika yasiyofuata sheria ukagonga mwamba iwapo utaendeshwa kisiri.

Bunge na asasi nyinginezo ambazo zimekuwa zikichunguza sakata ya mateso ughaibuni wamebaini kwamba ukosefu wa sheria thabiti pia ni miongoni mwa masuala yanayochangia Wakenya wanaofanya kazi za nyumbani kuendelea kuteseka katika nchi za kigeni.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Rais amjaribu Nelson Marwa kukabili...

Mbunge adai watu mashuhuri Mlima Kenya wamepiga jeki Raila...

T L