• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
TAHARIRI: Serikali itilie mkazo elimu ya wanafunzi wa Gredi ya 7

TAHARIRI: Serikali itilie mkazo elimu ya wanafunzi wa Gredi ya 7

NA MHARIRI

RIPOTI zimeibuka kuwa wanafunzi wa Gredi ya 7, ambao ndio waasisi wa mfumo mpya wa elimu (CBC), hawafundishwi ipasavyo kutokana na changamoto nyingi.

Changamoto kuu kati ya hizo ni uhaba wa walimu. Kwamba serikali inategemea mwalimu mmoja au wawili walioajiriwa majuzi na tume ya TSC, kufundisha wanafunzi wa daraja hiyo.

Baadhi ya shule, tukirejelea shule za umma, imeripotiwa kuwa wanafunzi wanafunzwa masomo mawili pekee kwa sababu shule husika zina mwalimu mmoja au wawili walioidhinishwa kufundisha Mtaala wa Umilisi (CBC).

Walimu wengine, ambao hapo awali waliruhusiwa kufundisha darasa la 7 na 8 hawaruhusiwi kuwafunza wanafunzi wa Gredi ya 7.

Tukio kama hilo linaonyesha kuwa serikali ina uzembe wa kufanikisha harakati rahisi. Hii ni kwa sababu mtaala wa CBC, japo ni tofauti na 8-4-4, kwa kiwango kikuu tofauti si kubwa sana.

Kwa hakika, hata katika baadhi ya mada zinazofunzwa katika masomo kama vile Kiswahili, kazi ya mwalimu imerahisishwa kwa kuzisongesha mada ‘ngumu’ au changamano hadi katika madarasa ya baadaye.

Kutokana na uhaba huo wa walimu, aidha pana hali ambapo mwalimu mmoja anafunza zaidi ya masomo matatu. Inaelezwa kuwa utampata mwalimu aliyesomea, kwa mfano, Hisabati na Jiografia, akifunza masomo mengine asiyoyajua vyema katika taaluma yake ya ufundishaji.

Hii ina maana kuwa wanafunzi hawafunzwi vyema na kuielewa mada inayoshughulikuwa kwa kuwa mwalimu anayefunza hana umilisi wa kumudu mada husika.

Wanafunzi wa Gredi ya 7, 8 na 9, wamepewa masomo 13 ya kushughulikiwa. Kwa hivyo unapolinganisha idadi hiyo ya masomo na walimu (mmoja au wawili), basi unabaini kuwa kuna tatizo kubwa.

Mbali na changamoto hizo za walimu, pia shule nyingi za umma hazina miundomsingi ya kimsingi inayohitajika ili kufanikisha CBC.

Mfano ni shule nyingi hazina maabara, maktaba na hata vitabu vya kiada vinavyohitajika katika kufaulisha ufunzaji.

Serikali ifanye nini basi? Kwanza walimu wa P1 wa shule za msingi waruhusiwe kufunza watoto wa Gredi ya 7 na hata 8 mwakani.

Pili, walimu hao waandaliwe kozi fupi mashinani za kuwawezesha kufunza wanafunzi wa Gredi ya 7 na 8. Kwa kweli kinachohitajika kwa walimu hao ni namna ya kufundisha bali si mada ya kufundisha. Tatu serikali iajiri walimu zaidi, iharakishe mpango wa kujenga maabara na maktaba pamoja na kusambaza vitabu vya kiada kwa kila shule ya umma kwa haraka.

  • Tags

You can share this post!

Bola Tinubu wa chama tawala APC achaguliwa kuiongoza Nigeria

CECIL ODONGO: Ni unafiki serikali kutaka Raila awekewe...

T L