• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
TAHARIRI: Serikali iwapatie mafunzo mahasla watakaokopa pesa za Hustler Fund

TAHARIRI: Serikali iwapatie mafunzo mahasla watakaokopa pesa za Hustler Fund

NA MHARIRI

UZINDUZI wa Hazina ya Hustler jana Jumatano sasa unawapa matumaini mamia ya mama mboga, wanabodaboda na wafanyibiashara ndogo kujiendeleza kiuchumi.

Pesa hizi zitawasaidia wengi ambao huenda hali ngumu ya kiuchumi imewasukuma kutafuta usaidizi kutoka kwa taasisi au watu binafsi wanaokopesha kwa masharti magumu.

Kupitia mkopo wa Hazina ya Hustler, watu wenye mapato ya chini wataweza kujaliza kwenye mtaji.

Kinachopendeza katika mpangilio huu ni kwamba wanaotaka pesa hizo watazipata kwa kuandika *254# na kuweka maelezo kidogo.

Wakati huu maelfu ya watu wamekwama katika madeni. Mbali na wanaodaiwa na apu mbalimbali za simu, wapo wengi wanaokopa pesa kutoka kwa watu binafsi wanaojulikana maarufu kama ‘shylock’ wanaotoa pesa zao kwa riba ya juu.

Tofauti na mikopo mingine, wanaokopeshwa na Hazina ya Hustler watawekewa akiba pamoja na malipo ya uzeeni. Mtu akiomba pesa kwa mfano Sh1,000, atapewa Sh950. Hizo Sh50 za juu zitagawanywa kwa makundi mawili. Sh35 zitawekwa kama akiba yake huku Sh15 zikiwa sehemu ya bima yake ya uzeeni.

Ina maana kuwa kwa watu wasiokuwa na mpango wa malipo kama wa NSSF, watakuwa moja kwa moja wanajiwekea akiba.

Katika kuchukua mkopo huu, jambo moja linalojitokeza ni kwamba kamwe si pesa za kutumiwa kwa mahitaji mengine isipokuwa biashara. Pesa hizi hutakikana kulipwa baada ya siku 14 pekee. Iwapo mtu atakuwa amechukua na azitumie kwa anasa au matumizi ya kibinafsi, kuna uwezekano mkubwa kuwa atakuwa hajapata pesa nyingine siku ya kuzilipa.

Kwa sababu hii, mbali na masharti na kanuni za hazina hiyo, ipo haja kwa serikali kuja na mpango wa kuwaelimisha watu wa mapato ya chini jinsi ya kujiendeleza kiuchumi.

Waziri wa Vyama vya Ushirika, Bw Simon Chelugui anapaswa kuweka sera ya kuwapa mafunzo wanaolengwa kunufaika na mikopo kutoka kwa Hustler Fund. Mafunzo hayo yanapaswa kuangazia jinsi ya kuanzisha biashara kutumia pesa kidogo.

Mafunzo hayo yatawasaidia watu wasiokuwa na uwezo wa kifedha lakini wenye maono ya kuwa na biashara zao.
Pia kuna wale walio na biashara tayari lakini hawajui jinsi ya kuzipanua.

Kupitia mafunzo kama hayo, itakuwa rahisi kwa watu kutumia vizuri mikopo yao kupanua biashara zao, na hatimaye kuwapa wengine ajira.

Kwa kufanya hivyo, wanaokopeshwa watamudu kuendeleza biashara zao na kupata urahisi wa kulipa mikopo yao kwa wakati unaofaa.

Hazina hii itakuwa na manufaa sio tu kwa walengwa, bali nchi nzima kwa jumla iwapo hali ya uchumi itaimarika kwa watu wa mapato ya chini.

You can share this post!

Viongozi wataka Gachagua akamilishe miradi Mt Kenya

JURGEN NAMBEKA: Vijana watangamane na wanaowafaa msimu huu

T L