• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Serikali yafaa imalize wizi wa chakula cha msaada

TAHARIRI: Serikali yafaa imalize wizi wa chakula cha msaada

NA MHARIRI

TAKWIMU zinazojitokeza kuhusu hali ya kiangazi nchini ni za kusikitisha.

Ziwa Turkwell katika Kaunti ya Turkana ni la punde zaidi kukauka, na kuweka hatarini maisha ya maelfu ya watu. Katika sehemu mbalimbali za nchi, mimea imekauka na sura za watoto walio na utapiamlo zinasikitisha. Idadi kubwa ya watu wako katika hatari ya kufa njaa na kiu, iwapo hakutanyesha ndani ya wiki chache zijazo.

Kama taarifa ya Idara ya Utabiri wa hali ya Anga ni za kuaminika, basi hapana bud kwa nchi kujiandaa na kipindi kirefu cha kiangazi. Hali hii inapoendelea, kuna hatari kubwa kuwa huenda watoto wa kike kutoka baadhi ya jamii wakaendelea kuingizwa kwenye ndoa za mapema.

Wasichana wengi Kaunti ya Kajiado wameanza kuolewa, ili wazazi wao wapate mahari ya kuwawezesha kuhimili makali ya njaa na kiangazi kwa siku chache. Kulingana na idara ya Watoto katika kaunti hiyo, wazazi wa wasichana hao wa umri mdogo, wamekufa mioyo kutokana na hali ya umasikini unaochagiwa na kiangazi hicho.

Baadhi ya wazazi hao wamepoteza mamia ya mifugo, na sasa hawana namna ya kujikimu wala kukidhi mahitaji ya familia zao. Wanaelewa kwamba kuwaoza watoto ni kinyume cha sheria. Lakini ni nani wa kuwashika mkono?

Baraza la Mawaziri Jumanne lilipitisha matumizi ya Sh4 bilioni kukabiliana na athari za kiangazi nchini.

Mawaziri walikubaliana kwamba kiangazi ni janga linalohitaji kukabiliwa kwa haraka. Juhudi zote zastahili kuelekejwa kwa kuweka mazingira bora ya watu kuepukana na athari hizo.

Ripoti iliyowasilishwa kwa baraza hilo la Mawaziri inaonyesha kwamba waathiriwa wakuu katika kiangazi hili ni watoto. Shule nyingi zimefungwa maeneo kame, ambako magavana hawajaanzisha mpango wa kuwapa wanafunzi chakula. Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ilitangaza kuwa itatoa msaada wa Sh16 bilioni. Mbali na pesa, shirika hilo litatoa msaada wa chakula kwa waathiriwa.

Usaidizi huu wa serikali na wahisani utakuwa na maana tu iwapo utawafikia walengwa. Kutenga pesa ni jambo moja.

Kutekeleza malengo ya pesa hizo ni jambo jingine. Serikali ina bahati kuwa licha ya kushamiri ufisadi, bado kuna watu wanaoiamini na kuisaidia wakati wa dhiki.

Kujitolea kwa USAID si jambo dogo, ikizingatiwa kuwa mashirika ya kigeni yana taarifa kuhusu tunavyofuja pesa zetu kwa ufisadi.

Ili kudumisha heshima ya nchi yetu, na kuonyesha kuwa kweli tunawajali watoto, wanawake na wakongwe walio katika hatari ya kufa kwa njaa, ni lazima safari hii tukomeshe wizi wa misaada hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Upinzani nchini Nigeria wapinga matokeo ya urais

JURGEN NAMBEKA: Vijana wa Pwani wajifunze kuhusu utaalamu...

T L