• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
TAHARIRI: Si busara serikali kurudisha ada za benki kwa wateja watumiao simu

TAHARIRI: Si busara serikali kurudisha ada za benki kwa wateja watumiao simu

NA MHARIRI

TANGAZO la Benki Kuu ya Kenya (CBK) kwamba wateja wataanza kutozwa ada ya kutoa pesa kutoka kwa benki hadi simu zao linajiri wakati usiofaa.

Kupitia tangazo, benki Kuu inasema afueni waliyopewa wakenya wakati wa kuingia kwa janga la Covid-19 itaondolewa ifikapo Januari 01, 2023.

Kwamba kufikia wakati huo, wateja watalazimika kulipa gharama ya kutoa pesa kutoka kwa benki au hadi kwenye simu na kinyume chake.

Hata hivyo, ada hiyo itapunguzwa ikilinganishwa na iliyokuwepo kabla ya kusimamishwa.

Ingawa wakati wa kuondoa malipo hayo serikali ilisema ilikuwa ni kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama ya maisha kutokana na ugonjwa wa Corona, Benki Kuu inasema sababu hasa ilikuwa kuvutia wateja wengi zaidi kukumbatia matumizi ya huduma za benki kupitia simu zao.

Katika kipindi hicho, takwimu za CBK zinaonyesha kwamba idadi ya wateja wanaotumia huduma za pesa kupitia simu iliongezeka kwa zaidi ya watu milioni sita.

Hii iliongeza mapato ya watoaji huduma za kuweka na kutoa pesa kutoka Sh157 bilioni hadi zaidi ya Sh800 bilioni.

Kama hali ni hii, basi maswali mengi yanaibuka kuhusu hekima ya kurejesha ada za benki.

Hata baada ya kuondolewa ada hizo, faida za benki na watoaji wengine wa huduma za pesa kupitia simu zilipanda. Kwa hivyo hakuna hasara yoyote kuendelea kuwapa wateja huduma hizo kwa gharama nafuu. Ni nini hasa kinachosukuma CBK kubadili msimamo wa awali wakati ushahidi unaonyesha hakuna anayepata hasara?

Kurejesha ada hizo huenda kukaathiri mapato ya watoaji huduma, ikizingatiwa kuwa huenda watu wakawa wakifanya angalau shughuli moja au mbili kwa mwezi, ikilinganishwa na sasa ambapo wanafanya mara kwa mara.

Benki na kampuni za simu tayari zinapata pesa kupitia huduma za kutoa kwa ATM au ndani ya benki, na zile za M-Pesa, Telkom au Airtel Money.

Mtindo huo ungedumishwa wakati huu ambapo kila mtu analalamikia gharama ya juu ya maisha.

Mamilioni ya Wakenya wanaendelea kutegemea chakula cha msaada. Kuna wengi wanaopoteza ajira kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kupungua kwa biashara.

Wenye makampuni huenda wakafunga mapema kwa msimu wa Krismasi na Mwaka Mpya kwa kukosekana watu wenye uwezo wa kifedha kununua bidhaa na kutafuta huduma.

Shule zitakapofunguliwa Januari, wazazi wengi watakaokuwa na hela kidogo za karo ya shule, watataka kulipa kupitia simu zao. Ada hizo zitakuwa gharama ya ziada inayoweza kuepukwa kwa sasa, hadi hali ya uchumi itengenee.

You can share this post!

Vita baridi ndani ya Kenya Kwanza

Arati akana madai ya uhasama na Seneta Onyonka

T L