• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
TAHARIRI: Uchunguzi wa Shakahola usivurugwe kivyovyote

TAHARIRI: Uchunguzi wa Shakahola usivurugwe kivyovyote

NA MHARIRI

UCHUNGUZI kuhusu vifo vya watu zaidi ya 100 katika kijiji cha Shakahola, Kaunti ya Kilifi, umeingia katika awamu muhimu ya upasuaji wa miili.

Upasuaji huo ulioanza jana Jumatatu unatarajiwa kubainisha mambo mengi ambayo wananchi wamekuawa wakijiuliza kufikia sasa, kuhusu maafa hayo ya kutisha.

Uchunguzi huo wa miili utakuwa ukifanywa huku mamia ya familia zikiendelea kutafuta wapendwa wao wanaoaminika walikuwa waumini wa dhehebu la mhubiri Paul Mackenzie, ambaye yuko kizuizini.

Wakati huo huo, utafanyika pia kukiendelea kuibuka hatua nyingine tofauti ambazo zinapangiwa kufanya uchunguzi sambamba na ule wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI). Kufikia sasa, asasi ambazo zimetangaza mipango ya kufanya uchunguzi wa kando ni Seneti na Afisi ya Rais.

Katika Seneti, imesemekana kuna jopo ambalo litachunguza kisa hicho huku pia Rais William Ruto, akitangaza mipango sawa na hiyo.

Ijapokuwa huenda ikawa kuna nia njema katika hatua hizo za kuanzisha uchunguzi tofauti na ule wa polisi, inahitajika hatua hizi zifanywe kwa tahadhari kuu.

Katika miaka iliyopita, Kenya iliwahi kuwa na majopo mingi ya kuchunguza visa mbalimbali lakini hakuna mengi ambayo hutokea baada ya ripoti kuwasilishwa.

Ingekuwa bora zaidi kama polisi wangepewa muda na rasilimali za kutosha kufanya uchunguzi wao kwa njia huru ili haki itendeke kwa waathiriwa wote wa mkasa wa Shakahola.

Hatukatai kuwa, kumekuwepo wakati ambapo idara ya polisi hulaumiwa kwa utepetevu katika upelelezi wa uhalifu. Hakika, hata katika kisa hiki cha vifo vya halaiki Shakahola, polisi wamejipata lawamani kwa kuzembea kwani imefichuka kwamba ripoti zilikuwa zikitolewa mara nyingi kwao kuhusu dhehebu linalokiuka haki za binadamu.

Hii imekuwa kwa kiasi kwamba, mabadiliko yalifanywa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, kwa uongozi wa polisi Kilifi.

Licha ya hayo, Waswahili husema kuwa, wapishi wengi huharibu pilau.

Kwa hivyo, badala ya kuanzisha majopo mengi ya uchunguzi kwa wakati mmoja, hatua bora itakuwa ni kwa asasi husika za serikali kukaza kamba ili kuhakikisha polisi wanatekeleza wajibu wao kikamilifu wakati huu.

Vilevile, kuwe na uwazi kwa wanahabari na mashirika ya kutetea haki za binadamu kufuatilia kisa hicho na kukusanya habari ili kuhakikisha hakuna yeyote atakayejaribu kukwepa mkono wa sheria.

  • Tags

You can share this post!

Maandamano kufanywa nje ya makazi ya Uhuru

Ruto arusha ahadi zaidi

T L