• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
TAHARIRI: Usimamizi wa fedha za kaunti ukazwe zaidi

TAHARIRI: Usimamizi wa fedha za kaunti ukazwe zaidi

NA MHARIRI

SERIKALI za kaunti zitalazimika kutafuta mbinu za usimamizi wa fedha iwapo magavana wanataka kujitolea kutimiza ahadi zao kwa wananchi.

Kwa takriban miaka 10 iliyopita tangu serikali 47 za ugatuzi zianzishwe, kumekuwa na mivutano kati ya magavana na serikali ya kitaifa kuhusu fedha.

Magavana wamekuwa wakilalamika karibu kila mwaka kuhusu kucheleweshewa mgao wa fedha kutoka kwa serikali ya kitaifa.

Kulingana nao, hii huwa ni mojawapo ya sababu zinazowatatiza kutekeleza utoaji huduma bora inavyotarajiwa na wananchi.

Hata hivyo, wakati mwingine huwa ni vigumu kwa raia kuelewa wanachomaanisha magavana hao kwa sababu mbalimbali.

Kwanza, kuna kaunti ambazo hukusanya mamilioni ya pesa kila mwezi kutoka kwa kodi za kibiashara ilhali haieleweki wazi jinsi fedha hizo hutumiwa.

Utapata wafanyabiashara wadogo sokoni wakilipa kodi zao kwa uaminifu kila siku, wiki au mwezi, kulingana na inavyotakikana kwa sheria za kaunti zao ilhali masoko hayo ni machafu, hujaa tope wakati wa mvua na hayana rasilimali muhimu kama vile vyoo na maji.

Katika sekta ya uchukuzi wa umma ambayo ni miongoni mwa zinazotolea kaunti kodi tele, utapata hakuna vituo vya kuridhisha vya magari ya umma ambapo kaunti inatoza kodi.

Hali hii hurejelewa katika sekta nyingine za kibiashara zinazohitaji huduma za kaunti ilhali haziridhishi licha ya fedha zinazokusanywa.

Mbali na haya, raia hujionea jinsi kuna wafanyakazi wengi katika serikali za kaunti ambapo baadhi yao hata haijulikani kazi wanazofanya.

Baadhi ya wafanyakazi hawa huwa maarufu kwa kuishi maisha ya kifahari, wengine wakitajirika haraka punde baada ya kuajiriwa katika vyeo visivyoeleweka.

Inaeleweka kwamba magavana wana kila haki ya kuitisha mgao kamili wa fedha ambazo zinafaa kutolewa na serikali ya kitaifa.

Lakini pia, magavana wanahitaji kufahamu kuwa hakuna mabadiliko yatakayopatikana iwapo wataendelea kufuata mkondo wa watangulizi ambao hawakujali kuhusu matumizi bora ya fedha.

Kaunti zitafanikiwa kuvutia uwekezaji zaidi wa kibiashara iwapo zitajitolea kuboresha mandhari za biashara hizo.

Hii haitawezekana ikiwa kodi zinazokusanywa zinaishia mifukoni mwa watu wachache.

Vilevile, fedha nyingi zinazopotezwa kwa mishahara na marupurupu ya vyeo ambavyo havisaidii wananchi zinaweza kuhifadhiwa kwa maslahi ya umma.

Fedha hizi zielekezwe kwa miradi ya kutolea wananchi huduma bora badala ya kutuza wandani wa watu wenye ushawishi katika kaunti zetu kwa kuwaundia afisi kiholela.

You can share this post!

Manufaa ya karkadi (hibiscus)

Mwanahabari kortini kwa madai ya kubeba gruneti

T L