• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 2:08 PM
TAHARIRI: Usimamizi wa raga ulainishwe ili kuinua ubora

TAHARIRI: Usimamizi wa raga ulainishwe ili kuinua ubora

NA MHARIRI

TIMU ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu Kenya Shujaa imehangaika kwenye Raga za Dunia za msimu 2022-2023.

Imevuta mkia katika duru za Hong Kong I na Los Angeles. Haijafika robo-fainali kuu katika duru sita mfululizo na kuzua hofu miongoni mwa mashabiki wake ndani na nje ya Kenya.

Vijana wa kocha Damian McGrath walipiga Australia pekee katika mechi yao ya kwanza ya Los Angeles Sevens nchini Amerika kabla ya kupoteza dhidi ya Fiji, Japan, Canada na Amerika.

Walipoteza nafasi kubwa sana ya kuingia robo-fainali kuu walipoduwazwa na wanyonge Japan katika mechi yao ya mwisho ya makundi na kuishia kuambulia pointi moja.

Shujaa walishuka kutoka nafasi ya 12 hadi 13 katika ligi hiyo ya mataifa 15. Nambari 15 watateremshwa daraja moja kwa moja baada ya duru ya 10 mjini Toulouse, Ufaransa.

Nambari 12, 13 na 14 baada ya Toulouse Sevens zitaingia mashindano ya mzunguko kuamua timu zaidi zitakazoshushwa yatakayojumuisha timu nne pamoja na mshindi wa Challenger Series 2023 mwezi Mei.

Timu mbili za kwanza katika mzunguko zitatinga fainali na kisha mshindi kupandishwa daraja kushiriki Raga za Dunia 2024 zitakazohusisha mataifa 12, huku hizo timu tatu zingine zikiangukiwa na shoka.

Shujaa iko mjini Vancouver, Canada kwa duru ya saba kwenye Raga za Dunia za 2022-2023.

Mara ya mwisho Shujaa ilikamilisha msimu bila kufika robo-fainali ni msimu 2010-2011 ilipoponea tundu la sindano kutemwa baada ya washiriki wa duru zote kuongezwa kutoka 12 hadi 15.

Matokeo mabovu msimu 2022-2023 yanasemekana kutokana na madai ya usimamizi mbaya katika Shirikisho la Raga Kenya (KRU).

Ni mwezi uliopita tu wakati Mahakama ya kusikiliza kesi za michezo (SDT) ilifutilia mbali uchaguzi wa maafisa Joshua Aroni (mweka hazina), Ian Mugambi (katibu) na Oscar Mango (mkurugenzi) na kumkaripia Msajili wa Michezo Rose Wasike kwa kuharibu uchaguzi wa Septemba 2022.

Huku KRU ikijiandaa kwa uchaguzi wa kitaifa baadaye mwezi huu (Machi 24) mjini Nairobi, ni muhimu isafishe nyumba yake.
Uchaguzi uendeshwe kwa ustaarabu. Ufuate sheria za michezo. Maslahi ya wachezaji na benchi ya kiufundi lazima pia yazingatiwe ili kuepuka visa vinavyoharibia KRU jina na kusababisha wadhamini kuhepa.

Shujaa imekuwa katika Raga za Dunia tangu 2002-2003. Bila ya usimamizi mzuri itakuwa vigumu Shujaa na raga ya Kenya kwa jumla kupiga hatua nzuri.

Ni muhali waziri wa Michezo kumlika spoti hii ili kuhakikisha viwango vya havidorori wakati malengo yake na azma yake kuu ni kuinua vipawa na sanaa, michezo yote nchini.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Nigeria ni mfano bora kuwa mtu mui hatimaye...

Mamia wala mbwa, mizizi kuzima njaa

T L