• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
TAHARIRI: Viongozi wa siasa waache misimamo yao mikali

TAHARIRI: Viongozi wa siasa waache misimamo yao mikali

NA MHARIRI

MUUNGANO wa Azimio la Umoja One Kenya, jana Jumatatu ulitimiza mpango wake wa maandamano katika miji mbalimbali nchini.

Maandamano makubwa zaidi yalifanywa katika jiji kuu la Nairobi ambapo fujo zilitokea katika sehemu tofauti kwa makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa upinzani.

Kupitia kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, serikali ya kitaifa ilikadiria kuwa, hasara ya takriban Sh2 bilioni zilipatikana kwa sababu ya maandamano hayo.

Ingawa takwimu hizo hazijathibitishwa kwa njia huru, kilicho wazi ni kuwa biashara nyingi ziliathirika mbali na shughuli nyingine nyingi za kawaida katika maeneo ambapo maandamano yalifanywa.

Kuna shule kadhaa hasa za jiji kuu ambazo wazazi waliarifiwa wasipeleke watoto wao jana Jumatatu kwa hofu ya ghasia.

Vilevile, nchi kama vile Uingereza ilitoa ilani kwa raia wao kuwatahadharisha kuhusu hali ya usalama kwa sababu ya maandamano, hali inayoweza kuathiri utalii nchini.

Hatukatai kwamba Katiba imewapa wananchi uhuru wa kuandamana kutetea haki zao. Hata hivyo, inafaa ieleweke kuwa, kama kuna njia mbadala inayoweza kuleta haki hizo, njia hiyo inafaa kufuatwa ili kuepusha hasara zinazosababishwa na maandamano.

Kufikia sasa, vinara wa Azimio wakiongozwa na Bw Odinga wameshikilia vikali matakwa yao kwa serikali wanayodai iko mamlakani kiharamu.
Kwa upande mwingine, serikali ikiongozwa na Rais William Ruto, pia imeshikilia msimamo wake kwamba haitashauriana na viongozi ambao, kulingana na serikali, wanataka kukiuka Katiba.

Pande zote mbili zinastahili kutafakari kuhusu maslahi ya nchi na kuweka kando matamanio ya kibinafsi. Haya yatawezekana tu iwapo viongozi watakubali uhalisia wa mambo yalivyo na watafute jinsi ya kulegeza misimamo yao.

Viongozi wa upinzani watambue kuwa, hakuna jinsi serikali itakubali matakwa yao yote wanayopigania kwenye maandamano.

Kwa upande mwingine, viongozi serikalini watambue kuwa wenzao wa upinzani wana ufuasi mkubwa kitaifa na pia, maoni yao hayafai kupuuzwa bila kupewa nafasi mwafaka ya kujieleza.

Pande hizo mbili zikiendelea kujipiga kifua, kila mmoja akitaka kuonyesha ubabe wake, mwananchi anayedaiwa kupiganiwa haki zake ndiye ataendelea kuteseka.

Hakutakuwa na faida yoyote kuendeleza makabiliano haya kwa miaka mitano ijayo kabla Uchaguzi Mkuu mwingine ufanyike.

  • Tags

You can share this post!

Bayer Leverkusen yazamisha chombo cha Bayern Munich katika...

Polisi kuumiza raia wenye njaa ni kutia msumari moto kwenye...

T L