NA MHARIRI
TANGU Jumanne wiki hii, wabunge wanawake wamekuwa wakiendeleza uvaaji mavazi ya Kiafrika.
Kupitia chama chao (KEWOPA), wabunge hao wamekuwa wakivaa vitenge na mavazi mengine yanayoonekana kuwa yasiyo rasmi.
Kanuni za Bunge husisitiza kuwa wabunge wavae nadhifu na kwa njia inayoonyesha urasmi.
Wakati mmoja mwaka 2011, aliyekuwa mbunge wa Makadara, Bw Mike Mbuvi Sonko, alitimuliwa bungeni kwa kuvaa kipuli.
Ni juzi tu ambapo Spika wa Seneti Amason Kingi alimfukuza bungeni Seneta Maalum Karen Nyamu. Seneta huyo mwenye vituko alikuwa amevaa nguo iliyoacha wazi makwapa.
Ingawa vitenge na mavazi ya Kiafrika yaliyo nadhifu huruhusiwa bungeni, mpango wa wabunge wanawake kuvaa vitenge kwa wiki nzima si muhimu na wala si wa dharura kwa sasa.
Wabunge hao wanawake wamegeuza Bunge kama jukwaa la mashindano ya fasheni.
Kila mmoja anaposhindana kuonyesha mwenzake mishono, na nguo hizo zinavyowatoa warembo, masuala muhimu ya kitaifa yanayowahusu wanawake yanaendelea nchini bila mchango wao.
Vipindi vya BBC Africa Eye na Panorama vimeanika uozo wa dhuluma za kingono katika shamba la kukuza majanichai la kampuni ya Finlays.
Wanawake wamelazimishwa kujamiana na wasimamizi wao ili waajiriwe au wapewe majukumu rahisi kwenye shamba hilo la majani.
Wakati huu pia, uchunguzi wa Taifa Leo unaonyesha kuna idadi kubwa ya watoto ambao hawajajiunga na shule za upili.
Kati yao, wengi ni wasichana ambao wazazi hawana pesa za kuwapeleka shuleni, hata baada ya kupata alama nzuri kwenye mtihani wa KCPE.
Seneta Maalum Gloria Orwoba amewasilisha hoja ya kutaka kuwe na mpango wa kuwapa wasichana sodo bila malipo.
Badala ya kushindana kuvaa vitenge, wabunge hao wangetoa kauli za kushutumu dhuluma dhidi ya wanawake kwenye mashamba ya majanichai.
Leo hii wangefanya harambee kusanya pesa za kufadhili wasichana waingie kidato cha kwanza.
Uongozi wa wabunge si kutunga sheria peke yake. Kuna uwakilishi. Huu unahusu kuyaangazia masuala muhimu ya wasio na sauti katika jamii.
Itakuwa makosa sana kama kufikia mwisho wa kipindi cha kuvaa mavazi ya Kiafrika, wabunge wa kike chini ya KEWOPA hawatakuwa wamepeleka angalau wasichana 100 katika shule ya upili.
Kufanya kampeni ya kuvaa mavazi yanayotengenezewa humu nchini si jambo baya. Lakini itakuwa na faida gani kama watu wanaotakiwa kununua mavazi hayo, hawana hata uwezo wa kupeleka mabinti zao shuleni?
Kampeni hii ingefaa zaidi baada ya kutatua shida iliyo muhimu sana kwa wakati huu; ambayo ni elimu ya mtoto wa kike.