• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 11:20 AM
TAHARIRI: Wabunge wafaa waheshimu hadhi yao na kuonyesha kujali wananchi

TAHARIRI: Wabunge wafaa waheshimu hadhi yao na kuonyesha kujali wananchi

NA MHARIRI

KITENDO cha wabunge kushika mateka serikali huku wakiendelea kufuja pesa za umma ni cha aibu na kuudhi.

Wabunge 300 kwa zaidi ya siku mbili, walisusia vikao vya kuwaelimisha kuhusu shughuli za Bunge katika hoteli ya PrideInn mjini Mombasa.

Walidai kuwa ajenda ya kwanza iliyostahili kujadiliwa ni kupatikana kwa pesa za Hazina ya maeneo Bunge (NG-CDF). Pesa hizo wanazidai hata baada ya Mahakama ya Upeo kutoa msimamo wake mwaka jana kuwa si halali.

Uamuzi uliotolewa na Jaji Mkuu Matha Koome na majaji wenzake, ulisema kwa kuwa maeneobunge yako katika Kaunti, NG-CDF ilistahili kubadilishwa jina na pesa hizo ziwe zikipelekwa kwa akaunti za serikali za kaunti.

Wabunge hao walipuuza uamuzi wa mahakama na kuja na kisingizio kuwa CDF iliyoharamishwa ni ya sheria ya mwaka 2013 na wala si NG-CDF ya mwaka 2015 ambayo kwa mtazamo wao, ni halali.

Kiasi cha Sh4 bilioni ambacho serikali ilianza kuweka kwenye akaunti za maeneo bunge si pesa chache.

Kisingizio cha wanasiasa hao ni kwamba eti wazazi wengi masikini wanahitaji basari za watoto wao werevu. Haya ni madai yasiyo na ukweli.

Wabunge wengi wamekuwa wakilaumiwa kuwa hutumia basari hizo kulipiza kisasi dhidi ya watu wanaochukuliwa kuwa wafuasi wa wapinzani wao.

Wengine hutoa basari kwa jamaa zao au marafiki na kuwapuuza masikini wanaostahili zaidi mgao huo. Isitoshe, sasa hivi kaunti nyingi zina mpango wa kugawa basari, mbali na wakfu na benki mbali mbali kama vile mpango wa Wings To Fly wa benki ya Equity.

Wabunge hao, kwa kususia vikao tangu Jumatatu, waliendelea kudhihirishia ulimwengu kuwa wanasukumwa na maslahi yao. NG-CDF hutumika kama chombo cha kujipigia debe mashinani.

Wanasiasa wanapotafuta ubunge, hutoa ahadi za kufanya maendeleo, ilhali jukumu la mbunge ni uwakilishi na kutunga sheria pekee.

Kinachovunja moyo ni kuwa wabunge hao wanaendelea kulipwa marupurupu pamoja na gharama nyingine wakiwa hawajaanza shughuli ya mafunzo iliyowapeleka Mombasa.

Mafunzo ya sasa yanajiri baada ya mengine kama hayo katika hoteli ya Safari Park, Nairobi.

Ingawa ni muhimu kuipatia biashara sekta ya utalii, mikutano hii inayotumia mamilioni ya pesa za mwananchi, inafanywa kwa gharama kubwa wakati ambapo serikali inawataka watu wajifunge mishipi na kudhibiti gharama ya maisha.

Wabunge na wenzao maseneta ambao wameenda kwa mafunzo nje ya nchi, waelewe kwamba uwakilishi si lazima uje kwa gharama. Ni utoaji huduma bora kwa uwazi, bila mapendeleo bila kumuongezea mzigo mhudumiwa.

  • Tags

You can share this post!

Bunge lazimwa kuingilia mzozo wa umiliki ardhi

Serikali yaahidi kuwasaidia wakulima kuimarisha uzalishaji...

T L