• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
TAHARIRI: Wabunge wasitishe ulafi, wajali waathiriwa wa ukame

TAHARIRI: Wabunge wasitishe ulafi, wajali waathiriwa wa ukame

NA MHARIRI

RIPOTI kwamba wabunge, kupitia Tume ya Huduma ya Bunge (PSC), wanataka kushinikiza Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kuwarejeshea marupurupu iliyoondoa ni kilele cha ulafi hasa wakati mamilioni ya raia wanaowakilisha wanakumbwa na baa la njaa kufuatia ukame wa muda mrefu.

Ripoti hizo zinasema kwamba tayari wamepanga kuwekea presha SRC ili iweze kukubali matakwa yao bila kujali hali ambayo raia wa kawaidia waliowachagua ili waitwe waheshimiwa wanapitia.

Waheshimiwa hao wanafaa kuonyesha uheshimiwa zaidi kwa kusubiri hadi hali ya uchumi iimarike kabla ya kusukuma tume hiyo kuwarejeshea marupurupu ambayo iliondoa baada ya utafiti wa kina, na kwa lengo zuri la kupunguza gharama ya serikali ya kutumia asilimia kubwa ya mapato yake kulipa mishahara huku ikikosa pesa za kutekeleza miradi ya maendeleo.

Ingekuwa bora kama wangetafuta njia ya kikatiba ya kurejesha Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (CDF) ambayo, Wakenya wengi wanakubaliana kwamba ilisaidia sana raia wa kawaida katika maeneo wanayowasilisha.

Badala ya kutumia muda, nguvu na wakati wakipanga jinsi ya kushawishi SRC iwaruhusu kujaza akaunti zao na pesa, wangekuwa wakipanga jinsi ya kufanya hazina hiyo ilandane na Katiba ya Kenya ilivyoshauri Mahakama.

Hapa suala la kuheshimu Mahakama na tume huru pia linazuka.

Kinaya ni kwamba wanatoa shinikizo hizi wakati Rais William Ruto anarai wafadhili kusaidia serikali kuokoa maisha ya Wakenya 5.1 milioni wanaokabiliwa na hatari ya kufa njaa na wakati ambao ameagiza Wizara na Idara za serikali kupunguza matumizi ili kuokoa pesa.

Wabunge ambao wanawania pesa za mlipa ushuru ambazo hazitoshi kulipa madeni ya nchi, wanafaa kubadilisha nia, wasionekane kuwa maadui wa nchi na kutojaji maslahi ya raia wa kawaida waliowachagua.

Kisingizio kwamba wanategemewa sana na wapigakura wa maeneo yao hakifai kutumiwa kuhalalisha ulafi wao kamwe.

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Analenga kuwa profesa karibuni

WANTO WARUI: Kuna hatari serikali kujiondoa katika ufadhili...

T L