• Nairobi
  • Last Updated May 29th, 2023 9:37 PM
TAHARIRI: Wahalifu wote wa mauaji ya Shakahola wafichuliwe bila kusazwa

TAHARIRI: Wahalifu wote wa mauaji ya Shakahola wafichuliwe bila kusazwa

NA MHARIRI

MNAMO Jumanne, Mhubiri Paul Mackenzie alifikishwa kwenye mahakama ya Malindi na kusomewa mashtaka upya kabla ya kurejeshwa kizuizini siku 90 mahakamani Shanzu.

Leo ni siku ya pasta Ezekiel Odero ambaye anatarajiwa kujibu mashtaka kuhusiana na vifo hivyo vya watu zaidi ya mia ambao miili yao ilifukuliwa kwenye makaburi ya kijiji cha Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Maafisa wa Jinai kufikia sasa, wamepiga hatua kubwa kwenye uchunguzi wao hasa kupitia matokeo ya upasuaji ambao unaendelezwa kwa ushirikiano na Mwanapatholojia mkuu wa serikali.

Ufichuzi unaoendelea kutolewa umehuzunisha Wakenya mno hasa inapoibuka waziwazi kwamba wanyonge hasa watoto, wanawake na wazee ndio waliolengwa na wahalifu ambao waliwaua kwa kuwanyonga na kuwanyima chakula na maji.

Kundi hili la viumbe dhaifu liliteseka mikononi mwa watu waliotumia dini kuwapotosha kwa kuwahadaa kwamba wangefika mbinguni kupitia vifo hivyo vilivyojaa mateso, uchungu na dhuluma.

Kuna kila sababu ya wahalifu hawa wote waliojaa uafriti na unyama wa Ibilisi kusakwa popote walipo nchini na kufunguliwa mashtaka na hatimaye kuadhibiwa vikali kuendana na uhalifu walioutekeleza.

Kufikia sasa ni wahubiri wawili pekee Paul Mackenzie na Ezekiel Odera pamoja na wafuasi wao kadhaa ambao wamefikishwa mahakamani.

Kwa kutathmini uzito wa mauaji haya, bila shaka ni wahusika wengi waliofanikisha vitendo vyote vya uhalifu kutoka hatua ya kusaka, kuwavutia na kuwasajili waumini, kuwahubiria na kubadilisha imani zao, kuwashauri kufunga hadi vitendo vya kuwakaba koo, kuwagonga kwa vifaa butu ili kuwaua na hata hatimaye hatua ya kuwasafirisha na kuwazika makaburini hayo ya halaiki.

Isisahaulike kwamba kuna watu waliofahamu vitendo hivi vyote vya uhalifu kutoka hasa vile vilivyokuwa vikitekelezwa lakini hawakudhubutu kutoa habari. Hawa pia wanafaa kukabiliwa.

Isitoshe kuna maafisa wa serikali ambao kando na kufunika matukio haya pia walitelekeza majukumu yao ya kuwahakikishia wakazi usalama wao na kuzuia mauaji kama haya kuwakumba. Hawa pia wanapaswa kufichuliwa na kuchukuliwa hatua ifaayo.

Kama alivyowahakikishia Wakenya waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki, serikali inafaa kuweka wazi kila kitu kilichoendelea, na hasa wahalifu wote wote bila kusaza yeyote ili wachukuliwe hatua kali za kisheria ili wawe funzo kwa wengine.

  • Tags

You can share this post!

Mtoto niliyempata anakuja na bahati ya ushindi –...

‘Vyuo vikuu vya umma sasa ndio kusema’

T L