• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
TAHARIRI: Wanasiasa wasichochee umma dhidi ya wanahabari

TAHARIRI: Wanasiasa wasichochee umma dhidi ya wanahabari

NA MHARIRI

VITA dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari Kenya sasa vinaonekana kuanza kuchukua mkondo hatari zaidi.

Tangu serikali ya Kenya Kwanza ilipoingia mamlakani, vyombo vya habari vimekuwa vikilengwa kwa njia moja au nyingine.

Jana Jumatatu, wanahabari wa mashirika mbalimbali wakiwemo wa kampuni ya Nation Media Group walishambuliwa, kujeruhiwa na kuporwa mali zao walipokuwa wakikusanya habari kuhusu maandamano ya Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Wahalifu walioshambulia wanahabari hao hawakujulikana wazi mara moja ni wa mrengo gani wa kisiasa kwani, tofauti na maandamano ya wiki iliyopita, Jumatatu kulikuwa na wafuasi wa Kenya Kwanza ambao pia walijitosa mitaani kupinga wale wa Azimio.

Kwa muda sasa tangu serikali mpya ilipoingia mamlakani mwaka 2022, viongozi serikalini wamekuwa wakitoa matamshi ya chuki dhidi ya vyombo vya habari na wanahabari nchini.

Kumekuwa na maonyo mara kwa mara kutoka kwa wadau wa sekta ya uanahabari kwamba matamshi aina hiyo ni hatari kwa usalama wa wanahabari na pia kwa demokrasia na maendeleo ya nchi.

Hii ni kwa kuzingatia kuwa, vyombo vya habari hutegemewa sana kuangazia shughuli zote zinazoendelea serikalini na kitaifa kwa jumla bila kuegemea upande wowote.

Hivi majuzi, Mamlaka ya Mawasiliano nchini nayo pia ilijaribu kudhibiti utendakazi wa vyombo vya habari isivyofaa.

Hatua ya mamlaka hiyo ilichochewa na jinsi wanahabari walivyojitolea mhanga kupeperusha habari za moja kwa moja wakati wa maandamano ya Azimio wiki iliyopita.Kwa upande mwingine, upande wa upinzani nao pia ulijaribu kudhibiti jinsi habari za maandamano hayo zinapeperushwa, kwa kutaka wafuasi wake kususia shirika moja la habari nchini kwa madai ya kupendelea serikali.

Awali, baadhi ya viongozi serikalini wamewahi kutaja wazi wanahabari ambao wanadai wana chuki dhidi yao.Matamshi aina hii na vitendo hivi huhatarisha maisha ya wanahabari na rasilimali za mashirika ya habari.

Ni kutokana na uchochezi huu wa wanasiasa ambapo tumeanza kuona magenge ya wahalifu wakishambulia wanahabari mchana peupe.

Itakuwa hatari kama nchi hii itaachwa kurejelea enzi ambapo vyombo vya habari vilikuwa tu vipaza sauti vya serikali kwa kiwango cha kushindwa kukosoa maovu yaliyokuwa yakiwafaidi watu wachache wenye ushawishi serikalini huku mamilioni ya raia wakiendelea kuteseka.

  • Tags

You can share this post!

Wito wahubiri waeneze umoja

Kichaa cha kuiba mali ya familia ya Rais Mstaafu

T L