• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
FAUSTINE NGILA: Safaricom ikomeshe teknolojia ya kidole kwa M-Pesa, ni hatari

FAUSTINE NGILA: Safaricom ikomeshe teknolojia ya kidole kwa M-Pesa, ni hatari

Na FAUSTINE NGILA

LABDA hujasikia hili lakini linakuathiri moja kwa moja kwa kuwa wewe ni mteja wa M-Pesa. Majuzi rafiki yangu alimfaa mwenzake na simu yake ya mkononi ambayo ilikuwa na programu mpya ya M-Pesa.

Alifuta kila kitu kwa simu yake kabla ya kumpa rafikiye ambaye sasa alianza kupakua apu mbalimbali, M-Pesa ikiwano, kwenye Google Playstore na kuweka kwa simu hiyo mpya kwani yake ilikuwa na matatizo.

Saa chache baada ya rafiki yangu ambaye sasa alihamisha kadi ya simu kwa simu nyingine alianza kupokea jumbe kadha za M-Pesa.

Alianza kuona pesa zikitumwa kutoka kwa akaunti yake ya M-Pesa hadi nambari za watu wengine. Baadaye aligundua kuwa rafikiye aliyempa simu ndiye alikuwa akituma hela hizo.

Ingawa rafikiye alifikiri hela hizo zilikuwa zikikatwa kwa akaunti yake ya M-Pesa, alishangaa kuwa zilikuwa zikikatwa kwa akaunti ya rafiki yangu.

Hivi nikashangaa, mbona Safaricom wameunda apu mpya yenye matundu yanayoruhusu wezi kuiba hela za wateja? Mbona ikaweka teknolojia ya kidole kuhalalisha utekelezaji wa huduma zote za M-Pesa?

Hii inamaanisha kuwa mtu akiiba simu yako ya kisasa, au hata akiipata kibahati, anaweza kutoa apu ya M-Pesa, akaweka nyingine na kutumia kidole chake kuiba hela zote kwenye M-Pesa, M-Shwari, KCB M-Pesa n ahata Fuliza.

Ingawa teknolojia za kifedha hasa M-Pesa zimesaidia pakubwa kuinua uchumi wa nchi hii, ukosefu wa usalama wa kiteknolojia sasa unatishia kuondoa imani katika Safaricom.

Kote duniani, teknolojia ya kidole imekashifiwa kutokana na hali kuwa alama za vidole zonaweza kupigwa chapa kwa kutumia teknolojia za kisasa na kutumiwa kuiba pesa zilizo kwenye akaunti za benki au majukwaa ya kifedha mitandaoni.

Mwezi uliopita nilimsikia vizuri sana Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Sheila M’Mbijjewe akizionya benki na kampuni za kutoa huduma za kifedha dhidi ya kubuni teknolojia ambazo zinaweza pesa za wateja hatarini.

Hii inamaanisha serikali inajua kuhusu utovu wa usalama katika majukwaa ya kifedha mitandaoni, na kabla ya wezi wengi kutambua mbinu hii, kampuni zinazotoa huduma hizi zinafaa kuziba mianya hii.

Safaricom, kampuni kubwa sana hapa Afrika Mashariki, inafaa kutoa mfano kwa kampuni zingine zote, kwa kukomesha matumizi ya teknolojia ya kidole kwenye M-Pesa. Isisubiri kuagizwa na serikali.

Isisubiri hadi pale Wakenya milioni moja watalalamika kuwa hela zao zinaibwa, inafaa kuchukua hatua sasa.

Naelewa kuwa kuna shinikizo miongoni mwa kampuni kubwa kubuni teknolojia za kisasa kuboresha huduma kwa wateja, lakini ubunifu unaowaletea wateja tishio la kupoteza kila shilingi waliyohifadhi kwa M-Pesa unafaa kusimamishwa mwanzo.

Afadhali hata kutuma pesa kupitia kwa kadi ya simu kama kawaida kuliko kutumia apu mpya ambayo licha ya kukuonyesha kiasi cha pesa unachotuma na kupoteas kila mwezi, inaweza pesa zako hatarini.

Tunapobuni teknolojia, tuwe makini sana kwani tunaishi katika dunia iliyojaa wadukuzi na watu wasiopenda kutoa jasho. Tujue wahuni wamejaa mitaani na mitandaoni pia, hivyo tuwazime mapema.

 

Mwandishi ni mwanahabari wa teknolojia katika kampuni ya Nation Media Group. Pia, ni mhariri wa tovuti ya Taifa Leo. [email protected]; [email protected]

You can share this post!

Asukumwa jela miaka mitano kwa kudai pesa za fidia za mtu...

Chipukizi Appiah aanza kuona matunda ya uigizaji

T L