NA MHARIRI
ABAUTANI ya ghafla ya Katibu mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU) Bw Francis Atwoli na ya kulalamikia gharama ya juu ya maisha imechelewa.
Hii ni kwa sababu angefanya hilo mapema mara tu ugumu wa maisha ulipoanza kuwalemea raia na wafanyakazi wa nchi hii anaowakilisha.
Akiwa kwenye kikao cha kilicholeta pamoja vyama vya kutetea wafanyakazi duniani mjini Mombasa hapo Jumatano, Bw Atwoli alionekana kuilaumu serikali kwa kuongezwa kwa bei ya mafuta hali ambayo imesababisha gharama ya maisha na kupanda.
Jambo linaloshangaza hapa ni jinsi Bw Atwoli ameghutuka na kuanza kulalamikia kuongezwa kwa bei ya mafuta kana kwamba hii ndio mara ya kwanza bidhaa hiyo kufanyiwa mabadiliko hayo ya bei.
Baadhi ya wananchi wanashangaa kama kweli kiongozi huyu amekuwa akiishi humu nchini au la.
Ukweli ni kuwa hii si mara ya kwanza bidhaa hii kukwezwa bei mbali zaidi ya mara tatu huku Bw Atwoli akiwa kando akiwatazama wafanyakazi wakilemazwa na dhiki ya kiuchumi.
Mara ya mwisho bei ya mafuta ilipopandishwa, Wakenya wanakumbuka vizuri jinsi aliyekuwa waziri wa Biashara na Viwanda ambaye sasa ni waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria, alivyowazomea waliolalamika kwa kuwashauri wachimbe visima vyao vya mafuta ili waweze kujipatia mafuta ya bei nafuu.
Matamshi haya yalikosolewa na Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye alimtaka waziri huyo akome kuwatamausha zaidi Wakenya ambao walikuwa wakipitia changamoto za kiuchumi. Binadamu yeyote aliye na akili timamu atajiuliza, je, Bw Atwoli alikuwa wapi wakati huu?
Aidha, walipojumuika kwenye jukwaa moja na kinara wa Azimio Raila Odinga kwenye mkutano wa viongozi wa eneo la Maghariki, Bw Atwoli alipinga maandamano ambayo yalitumiwa na Upinzani kama mbinu ya kupinga mzigo wa gharama ya juu ya maisha uliosababishwa na serikali ya Rais Ruto.
Ni wakati huu ambapo Bw Odinga alimuonya Bw Atwoli dhidi ya kuwa upande mmoja na serikali raia wakizidi kuumia.
Bw Atwoli hafai kutumia ujanja na mbinu za kutuliza wafanyakazi tu ili asali kwenye kiti hicho chake. Ajitokeze kama shujaa wa kweli kutetea watu wake.
Wakenya sasa wanasubiri kumwona akiitisha kikao na serikali ya sasa ili wajadili jinsi watapunguzia raia mzigo wa maisha kama alivyoashiria.