• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
WANDERI KAMAU: Tuchunge ndimi zetu tunapoelekea 2022

WANDERI KAMAU: Tuchunge ndimi zetu tunapoelekea 2022

Na WANDERI KAMAU

KULINGANA na Ripoti ya Jaji Mstaafu Akilano Akiwumi (1997) kuhusu chimbuko la ghasia za kikabila nchini, wanasiasa ndio waliozianzisha katika miaka ya tisini.

Ripoti hiyo inadai ghasia hizo zilianza katika eneo la Miteitei, Kaunti ya Nandi, baada ya wanasiasa kuwashinikiza wenyeji kuzifurusha jamii ambazo zilionekana kuwa “wageni.

”Msukumo wa ghasia hizo ulitokana na mabadiliko ya kisiasa yaliyokuwa yakiendelea nchini, hasa baada ya marehemu Daniel Moi kufanya mabadiliko katika Kipengele 2 (a) cha Katiba.

Mabadiliko hayo yalitoa nafasi kwa uwepo wa vyama vingi vya kisiasa nchini.Baaada ya wanasiasa kufaulu kuwachochea wenyeji dhidi ya jamii hizo, ghasia hizo zilisambaa katika maeneo mengine ya ukanda wa Bonde la Ufa.

Baadhi ya sehemu zilizoathiriwa sana na machafuko hayo ni Enosupukia katika Kaunti ya Narok na Ol Moran katika Kaunti ya Laikipia.Kando na 1992, ghasia hizo zilishuhudiwa tena mnamo 1997, 2002 na 2007.

Mnamo 2007, Wakenya sita, wakiwemo Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto walifunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), baada ya zaidi ya Wakenya 1,300 kuuawa kikatili.

Bila shaka, wakati uhalisia mchungu kama huo unaendelea kudhihirika katika historia ya nchi yetu, inashangaza kuwaona viongozi wa kisiasa wakiendelea kutoa matamshi ya chuki bila kujali athari zake.

Narejelea matamshi yaliyotolewa juzi na mbunge Junet Mohamed (Suna Mashariki), kwamba ni jamii kutoka eneo la Nyanza pekee zitakazoshirikishwa kwenye serikali ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ikiwa ataibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Katika wakati huu ambao nchi inajitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa 2022, wanasiasa wanapaswa kutahadhari sana aina ya matamshi ambayo wanatoa.Ingawa mbunge huyo amejitokeza “kufafanua” alichomaanisha, wengi wanachukulia matamshi yake kwa uzito, ikizingatiwa yeye ni mshirika wa karibu sana wa Bw Odinga.

Si Junet pekee, bali tumekuwa tukiwaona washirika wa Naibu Rais William Ruto wakitoa matamshi sawia, baadhi hata wakitishia jamii ambazo zinaonekana kutomuunga mkono kwenye azma yake ya urais 2022.

Ni sikitiko kuu kwamba baada ya hali iliyoikumba Kenya kutokana na uchaguzi tata wa 2007, bado viongozi wetu hawajajifunza kuhusu jinsi chuki na ghasia za kikabila zinaweza kuiathiri nchi.

Je, wamejawa na upofu ama ni hali ya kutojali?Pengine ndilo swali linaloweza kuibuka, ikizingatiwa kwamba baadhi ya viongozi wanaoeneza chuki wamefanya ziara katika nchi zilizowahi kukumbwa na ghasia za kikabila kama vile Rwanda.

Si mara moja tumekuwa tukiwaona wabunge wakifanya ziara katika nchi mbalimbali duniani, wakidai “kujifunza” kutokana na matukio yaliyoyakumba mataifa hayo.Kulingana na tafiti kadhaa, matamshi ya wanasiasa na jumbe zilizotolewa na vyombo vya habari ndizo zilikuwa chanzo kikuu cha mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda mnamo 1994.

Kwenye mauaji hayo kati ya jamii za Wahutu na Watutsi, zaidi ya watu 800,000 waliuawa.Je, tumesahau yaliyowahi tukumba? Ni wakati tufunguke macho tusirejee tena katika enzi ya giza.

[email protected]

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Ruto, Raila watumie mitandao ya kijamii...

Upungufu mkubwa wa nyama wakumba Tana

T L