VIONGOZI wa kisiasa kutoka eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa wamemtaka Rais William Ruto kuwatuma wanajeshi wa Kenya (KDF) katika eneo la Bonde la Kerio na maeneo mengine yanayokumbwa na utovu wa usalama.
Wakiongozwa na Waziri wa Barabara na Uchukuzi Kipchumba Murkomen na kiongozi wa wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot, viongozi hao pia waliitaka serikali kuendesha shughuli ya kutwaliwa kwa bunduki kutoka kwa watu wanaozimiki kinyume cha sheria.
Lakini viongozi hawa wasije wakasahau kuwa kwa mujibu wa kipengele cha 241 (3) (c) cha Katiba ya sasa, Rais Ruto anaweza tu kutoa amri kama hiyo baada ya kupata idhini kutoka kwa Bunge la Kitaifa.
Hii ni tofauti na mnamo 2008 wakati ambapo Rais wa zamani Hayati Mwai Kibaki alituma KDF kukabiliana na wanachama wa wanamgambo wa Sabaot Land Defence Forces (SLDF) katika eneo la Mlima Elgon na wakafaulu kuzima maovu ya kundi hilo.
Kile Bw Cheruiyot na wenzake wanapaswa kufanya ni kuwasilisha hoja bungeni kumtaka Rais Ruto kutuma wanajeshi maeneo ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa kupambana na majangili.
Hoja kama hiyo itapita kwa urahisi kwani, kiidadi, Kenya Kwanza inadhibiti Bunge la Kitaifa na Seneti.