• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
VALENTINE OBARA: Wapwani waunge juhudi zote za kuhifadhi mikoko

VALENTINE OBARA: Wapwani waunge juhudi zote za kuhifadhi mikoko

NA VALENTINE OBARA

MNAMO Jumanne, wenyeji katika maeneo ya Pwani yanayopakana na bahari walijumuika na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha siku ya kimataifa ya kutunza mikoko.

Kwa kawaida, siku hii hutumiwa na wanamazingira kutathmini hatua zilizopigwa kufikia sasa katika uhifadhi wa mikoko, huku pia kukitolewa mapendekezo kuhusu kile kinachotakikana kufanywa katika siku za usoni.

Mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yameibuka katika miaka iliyopita kwa lengo la kuhifadhi mikoko; mimea muhimu mno kwa utunzaji wa mazingira ya bahari, kumaanisha pia ni muhimu kwa shughuli nyingine kama vile uvuvi.

Katika ukanda wa Pwani, hali ya hewa ambayo ni ya joto jingi inamaanisha hakuna misitu mingi inavyotakikana na hivyo basi, watunzaji mazingira huhimiza upanzi wa mikoko kujaza pengo lililopo.

Kwa bahati mbaya, umaskini umesababisha wakazi wengi kutegemea misitu hii kujikimu kimaisha.

Kumekuwa na ukataji mikoko ili kuuza mbao za miti hiyo ambazo husifiwa mno kwa utengenezaji wa fenicha, ujenzi wa nyumba miongoni mwa matumizi mengine.

Mbali na haya, kuna jamii ambazo zimekuwa zikikatakata mikoko kiholela huku sehemu zinazopakana na bahari zikigeuzwa mitaa ya mabanda.

Hata hivyo, mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo mengi ni makundi ya kijamii yametoa mchango mkubwa katika kurekebisha hali hii.

Makundi hayo ambayo mengi ni ya vijana na wanawake, hutoa mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mikoko, matumizi bora ya misitu hii kwa kupanda kiwango zaidi ya kile kinachokatwa, na vilevile, kuelimisha wananchi kuhusu jinsi wanaweza kujipatia mapato kupitia kwa upandaji na uhifadhi wa miti.

Licha ya haya, bado kuna changamoto zinazoibuka baina ya makundi haya.

Kwanza, kuna changamoto za kifedha ambazo hufanya makundi haya yasifanikishe malengo yao kwa kiwango ambacho kinaweza kunufaisha jamii zaidi.

Makundi mengi aina hii hutegemea wahisani kuendesha shughuli zao, hasa zile za kutoa hamasisho kwa jamii.

Mbali na haya, baadhi ya makundi huwa yameundwa bila kuwa na mfumo bora wa kiusimamizi.

Wito ni kwa wadau wengine wakuu, hasa idara za serikali ya kitaifa na zile za kaunti za Pwani zinazosimamia masuala ya mazingira, kuhakikisha kuna mipango ya kutosha kusaidia makundi haya ya kijamii yanayojitolea mhanga kuhifadhi mikoko.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali iepuke kuwasaliti raia kila...

BI TAIFA JULAI 28, 2022

T L