• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
TAHARIRI: Vizingiti vya mazungumzo viondolewe

TAHARIRI: Vizingiti vya mazungumzo viondolewe

NA MHARIRI

HATIMAYE kuna matumaini ya utulivu nchini baada ya pande mbili pinzani za kisiasa kuonyesha dalili za kupatana.

Jana Jumatatu, Serikali ya Kenya Kwanza chini ya Rais William Ruto iliwateua viongozi saba wa kisiasa watakaoshiriki mazungumzo na mrengo wa upinzani, Azimio la Umoja One Kenya, chini ya kinara wao Raila Odinga.

Hatua hiyo ilijiri siku nne baada ya mrengo wa Azimio kuwateua viongozi saba wa kisiasa kushiriki mazungumzo hayo yanayotarajiwa kumaliza uhasama na ubishani baina ya Kenya Kwanza na Azimio kuhusu masuala kadhaa. Mazungumzo haya yanatokea baada ya mrengo wa Bw Raila kuongoza maandamano mara tatu ambayo yalivuruga shughuli nyingi za kibiashara nchini hasa jijini Nairobi na kusababisha hasara kubwa na maafa.

Mbali na kuinyima serikali pato la takribani Sh3 bilioni kila siku ya maandamano, pia watu kadhaa walikufa na wengine kujeruhiwa vibaya. Inapozingatiwa kuwa serikali ya Kenya inakumbwa na tatizo kubwa la kifedha, kupotezea serikali jumla ya Sh9 bilioni ni hatari zaidi. Mrengo wa Azimio uliwataka wafuasi wake wafanye maandamano ili kushinikiza serikali ya Dkt Ruto kutekeleza matakwa mbalimbali.

Miongoni mwa matakwa hayo ni kufungua sava za uchaguzi mkuu uliopita ili kubaini mshindi halali wa urais, kupunguza gharama ya maisha hasa kwa bidhaa za kimsingi na kurejesha ruzuku zilizokuwapo wakati wa serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta, kusitisha mchakato wa kuajiri makamishna wa tume ya uchaguzi ya IEBC na kukoma kufifisha upinzani na demokrasia hasa kwa ‘kuwanunua’ wabunge wa Azimio.

Huku tukitarajia muafaka kupatikana kuhusu masuala haya tata, kuna ishara ya vizingiti vinavyoweza kuzuia mafanikio ya muafaka huo. Kwanza ni baadhi ya wafuasi wa mirengo hiyo kuonyesha misimamo mikali na kuanza kutoa matamshi ya kusambaratisha mapatano yoyote yanayoweza kutokea.

Uhalisia ni kwamba baadhi ya matakwa ya Azimio ni magumu kutimizwa lakini yasiposhughulikiwa ipasavyo huenda yakasababisha hasara kubwa zaidi ya kifedha na hata maisha.

Yamkini ni muhimu kuzingatia lengo kuu la mazungumzo hayo; kupatikana kwa amani na umoja wa Wakenya. Maslahi ya kibinafsi ya kisiasa yasiruhusiwe kuvuruga mchakato huu wenye umuhimu kwa taifa hili na ulimwengu kwa jumla. Amani huja na gharama.

Iwapo itabidi serikali igharimie amani inayotafutwa kupitia mchakato huu, basi heri gharama kuliko hasara. Pande zote mbili ziwashauri wafuasi kujiepusha na matamshi yoyote yanayoweza kuzuia maafikiano hayo kupatikana. Sharti Kenya isonge mbele kwa manufaa ya raia wake na wadau wengineo duniani kote.

  • Tags

You can share this post!

Waliopora mwanamke Sh50, simu wapewa bondi ya nusu milioni

Manchester City guu moja ndani ya nusu-fainali UEFA

T L