NA WANDERI KAMAU
LICHA ya matatizo kadhaa yaliyokumba utawala wake, mojawapo ya mafanikio aliyopata Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ni kubuni mazingira mwafaka ya kiuchumi kwa wawekezaji kutoka mataifa tofauti duniani.
Bw Kenyatta alifanya ziara zisizohesabika ughaibuni, katika juhudi za kuitangaza Kenya kama taifa lililo wazi kuwakaribisha raia wa mataifa tofauti kuwekeza humu nchini.
Ni hali iliyoifanya Kenya kupata sifa kubwa duniani kama taifa lililofungua milango yake kwa wawekezaji katika kila sekta.
Hilo, pia, liliifanya Kenya kuandaa makongamano makubwa makubwa ya kibiashara kama vile, Kongamano la Kimataifa la Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD), Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD.
Ni nyayo alizoahidi kufuata Rais William Ruto baada ya kuchukua uongozi kutoka kwa Bw Kenyatta.
Hata hivyo, inasikitisha kuwa baada ya kujitangaza duniani kama nchi inayowakaribisha raia wa kigeni kuwekeza na kuanzisha biashara zao, Kenya imeanza kuwapiga vita.
Hilo lilidhihirishwa juzi na hatua ya Waziri wa Biashara na Viwanda, Bw Moses Kuria, kuagiza kufungwa kwa kituo cha kibiashara cha China Square kilicho katika Chuo Kikuu cha Kenyatta mjini Nairobi. Sababu ya agizo lake? “Kwa kuwanyima biashara wafanyabiashara kutoka Kenya”.
Malalamishi hayo yametolewa kwani kituo hicho kimekuwa kikiuza bidhaa zake kwa bei za chini ikilinganishwa na wafanyabiashara wengine.
Ikizingatiwa kituo hicho kinamilikiwa na Wachina, wito mkuu wa serikali ni kuchukua hatua mbadala kuwalinda Wakenya badala ya kuwaingilia wawekezaji wa kigeni.