NA WANDERI KAMAU
UANAHABARI ni taaluma ambayo ina historia ndefu. Ni taaluma iliyoanzia katika mwaka 59BCE (Kabla ya Kuzaliwa Masihi Yesu Kristo).
Jarida la kwanza lililoandikwa lilianzishwa jijini Roma, Italia, ambapo liliitwa Acta Diurna. Jarida hilo lilikuwa likitumiwa kurekodi matukio muhimu katika jiji hilo na hotuba zilizotolewa na watawala tofauti wa Roma. Baada ya kukamilishwa kuandikwa, lilikuwa likiwekwa katika maeneo ya umma ili kusomwa na kila mmoja.
Baada ya hapo, taaluma ya uanahabari ilisambaa katika maeneo mengine duniani kama India, ilikopokelewa na kusifiwa sana na Wahindi.
James Augustus Hicky ndiye anayekisiwa kuwa mwanahabari wa kwanza duniani, kwani ndiye aliyeanzisha magazeti ya Bengal Gazzette na Calcutta General Advertiser mnamo 1870. Ndiye anayetajwa kuwa ‘baba wa uanahabari duniani’.
Bila shaka, urejeleo huo unaonyesha kuwa uanahabari ni taaluma yenye historia pevu na ndefu sana.
Si taaluma iliyoanza juzi, wala si taaluma iliyo katika nchi ama maeneo kadhaa. Ni taaluma ambayo imekuwepo kwa karne nyingi zilizopita.Hilo, bila shaka, linaonyesha kuwa uanahabari ni miongoni mwa taaluma kongwe sana duniani. Hilo, pia, ndilo limeiwezesha taaluma hiyo kupewa jina ‘Tawi la Nne’—baada ya matawi matatu makuu ya serikali kutokana na ukongwe wake.
Hivyo, inasikitisha kuona viongozi wa kisiasa kama vile Naibu Rais Rigathi Gachagua wakiwadunisha na kuwakashifu wanahabari kwa majukumu ambayo wanatekeleza.Tangu alipoapishwa kama Naibu Rais, Septemba 2022, Bw Gachagua ameonekana kubuni uhasama wa kimakusudi baina yake na vyombo vya habari.Amewasawiri wanahabari kama ‘maadui’ wa serikali na raia, ambao wamekuwa wakieneza uongo kuhusu matukio tofauti nchini.
Katika kisa cha juzi zaidi, Bw Gachagua aliapa kuanza “vita vikali” dhidi ya wanahabari kwa “kutomwelewa” na “kumharibia sifa”.
Bila shaka, mwelekeo huu ni hatari na ishara isiyoridhisha kwa mustakabali wa uhuru wa wanahabari na vyombo vya habari nchini.
Kwanza, ikiwa Bw Gachagua anahisi kukosewa na wanahabari au chombo fulani cha habari, kuna taratibu za kisheria na kikatiba ambazo anafaa kufuata katika kueleza malalamishi yake.
Kwa mfano, kuna Baraza la Vyombo vya Habari Kenya (MCK) ambalo huwa na kitengo ambacho hupokea malalamishi dhidi ya utendakazi wa wanahabari kutoka kwa raia, ama taasisi nyingine zinazohisi kukosewa kwa namna fulani na vyombo vya habari.
Pili, Bw Gachagua anaweza kuwahusisha viongozi wa chombo husika cha habari kwa kuelezea kutoridhishwa kwake na utendazi wa chombo hicho au mwanahabari husika.
Kando na hayo, kuna njia nyingine za kikatiba zilizopo anazoweza kutumia kuelezea malalamishi yake.
Hata hivyo, kuwakosoa na kuwashambulia wanahabari hadharani ni mwelekeo usiofaa, kwani matokeo yake ni kubuni mazingira yasiyofaa kwa utendakazi wao na uhusiano baina yao na raia.
Ni hali ambayo pia inahatarisha usalama wao.
Subscribe our newsletter to stay updated