• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
WANDERI KAMAU: Kawira Mwangaza ni mwathiriwa wa mitazamo duni ya jadi

WANDERI KAMAU: Kawira Mwangaza ni mwathiriwa wa mitazamo duni ya jadi

NA WANDERI KAMAU

JAMII ya Ameru ni miongoni mwa jamii ambazo zimekuwa zikimpa hekima na kumkweza mwanamume kama nguzo kuu ya uongozi wake.

Katika jamii hiyo, mwamamume huwa anapewa hekima kama kiongozi na mlezi wa jamii, anayefaa kushughulikia mahitaji ya familia yake —mke na watoto wake.
Ni sababu hiyo ambayo imelifanya Baraza la Wazee la Njuri Ncheke kuendelea kuwa na usemi na ushawishi mkubwa sana katika jamii hiyo, kuhusu masuala yanayohusu uongozi wa kisiasa na utatuzi wa mizozo baina ya watu wa kila tabaka.
Kijumla, jamii hiyo ni miongoni mwa chache zinazoendelea kudumisha tamaduni zilizokuwepo hapo awali miongoni mwa Waafrika, zinazotambua nafasi na mchango wa mwanamume katika jamii.
Hata hivyo, inasikitisha kuwa licha ya jamii na maeneo mengi nchini na duniani kote kukumbatia usasa katika masuala ya uongozi, wanaume wengi katika jamii ya Ameru wanaonekana kutotambua uhalisia huo.
Idadi kubwa ya wanaume katika jamii hiyo —hata waliosoma —wanaonekana kuendelea kukwamilia tamaduni za kizamani, zinazomsawiri mwanamke kama kiumbe dhaifu, asiye na uwezo wa kuwajibikia masuala na majukumu muhimu kama uongozi.
Sababu kuu ya urejeleo huu ni kuhusiana na matukio ambayo yamekuwa yakiendelea katika Kaunti ya Meru dhidi ya Gavana Kawira Mwangaza kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa.
Jumatano wiki iliyopita, Bi Mwangaza aling’olewa mamlakani, baada ya madiwani 59 kupiga kura ya kuunga mkono hoja ya kumrufusha kutoka uongozini.
Madiwani 10 walisusia upigaji huo wa kura. Kuna jumla ya madiwani 69 katika bunge hilo.
Licha ya hayo, ukweli ni kuwa kindani, masaibu yanayomwandama Bi Mwangaza yanatokana na misukumo ya kitamaduni inayomdunisha na kutomtambua mwanamke kama kiumbe mwenye uwezo wa kuiongoza jamii kisiasa.
Ingawa makala haya hayamtakasi Bi Mwangaza kwa maovu anayodaiwa kufanya, tashwishi kuu inayoibuka ni kuhusu “ukubwa” ama “ubaya” wa makosa hayo, kiasi cha kila mtu kumgeuka.
Hali ilivyo, Bi Mwangaza yuko peke yake. Ni kama mwanajeshi mmoja kwenye uwanja wa vita, anayewakabili wanajeshi 200!
Bi Mwangaza anakabiliana na Naibu Gavana Isaac Mutuma, Bunge la Kaunti, Baraza la Wazee la Njuri Ncheke, vigogo wa kisiasa katika kaunti hiyo kama Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na mwanasiasa mkongwe, Bw Kiraitu Murungi, aliyehudumu kama gavana kati ya 2017 na 2022.
Zaidi ya hayo, Bi Mwangaza hana uungwaji mkono wowote katika ngazi ya kitaifa, hasa baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kusema kuwa yeye na Rais William Ruto hawataingilia mizozo inayoiandama kaunti hiyo.
Alisema watawaruhusu watu wa Meru kusuluhisha changamoto zao wao binafsi. Hilo bila shaka linamwacha gavana huyo akijipigania mwenyewe.
Hata hivyo, hata ikiwa madiwani hatimaye watafulu kumwondoa uongozini gavana huyo (ikiwa uamuzi wao utaidhinishwa na Seneti), ukweli mchungu ni kuwa jamii hiyo iko kwenye kipindi kigumu cha mabadiliko ya kitamaduni na kisiasa, ambapo lazima iyakubali mabadiliko na mwelekeo huo mpya.
Nyakati ambazo mwanamke alionekana kuwa kiumbe dhaifu zimepitwa na wakati.
Lazima wanaume katika jamii ya Ameru wakubali uhalisia huo mchungu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

KCPE iliyoanza 1985 yafanywa kwa mara ya mwisho leo

Mwanaume niliyemkataa amenitusi eti nina kisima...

T L