• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
WANDERI KAMAU: Mzozo wa Urusi-Ukraine unatishia uthabiti duniani

WANDERI KAMAU: Mzozo wa Urusi-Ukraine unatishia uthabiti duniani

NA WANDERI KAMAU

DUNIA nzima inapoendelea kufuatilia kwa karibu mzozo kati ya Ukraine na Urusi, kile kinachoendelea kuibuka ni kuwa, mapigano hayo ni mvutano fiche ambao umekuwepo kwa muda mrefu kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi.

Mataifa ya Magharibi kama Amerika na Jumuiya ya Ulaya (EU), yamekuwa yakijaribu sana kuzikabili nchi zinazoonekana kuzipa ushindani kiuchumi, kisiasa na kijeshi. Mataifa ambayo yamekuwa yakilengwa hasa na Wamagharibi ni Urusi na China, kwa kuwa yameibukia kuwa yenye ushawishi mkubwa duniani katika miaka ya hivi karibuni.

Wamagharibi wamekuwa wakitishika sana na juhudi ambazo China na Urusi zimekuwa zikifanya kuimarisha usemi wake duniani, hasa kwa kuboresha ushirikiano na baadhi ya maeneo muhimu, kama bara Afrika. Imani ya Wamagharibi wengi— hasa Amerika na Uingereza— ni kuwa, ushawishi wa Urusi duniani uliisha kabisa 1990, baada ya kusambaratika kwa uliokuwa Muungano wa Mataifa ya Usovieti (USSR).

Amerika ndiyo ilifurahia sana kusambaratika kwa muungano huo, kwa kuwa ulionekana kuwa tisho kubwa kwa ushawishi wake wa kisiasa na kijeshi duniani. Kuvurugika kwa USSR ndiko kulikuwa mwisho wa Vita Baridi vya Dunia (1947-1990), ambavyo msingi wake mkuu ulikuwa ni mvutano wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi kati ya mataifa hayo mawili.

Licha ya “furaha” ya Amerika na washirika wake kutokana na “kifo” cha USSR, mzozo wa Ukraine unaashiria hofu ya Amerika kutoka kwa Urusi na China kupitwa kama taifa lenye uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi, kiuchumi na kisiasa duniani. Kwa sasa, China ndilo taifa linaloendesha miradi mingi barani Afrika ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika miaka ya tisini, ambapo Amerika na nchi za Magharibi zilikuwa zinaidhibiti Afrika katika kila hali—kisiasa na kiuchumi.

Hofu ya Amerika kupitwa kama taifa lenye uwezo mkubwa wa kijeshi duniani ndio ulioifanya kuvamia mataifa kama Iraq, Afghanistan na Libya, kwa kisingizio yalikuwa yakitengeneza silaha za kinuklia.

Kwenye uvamizi wa Iraq 2001, Amerika ilidai utawala wa marehemu Saddam Hussein ulikuwa na “kasha kubwa la silaha hizo.”

Amerika inahofia kuwa huenda isiwe rahisi kwake kuikabili Urusi kama vile ilivyofanikiwa kuyavamia mataifa mengine na kuvuruga chumi zake.

Hivyo, mzozo huu ni mchipuko mpya wa Vita Baridi vya Dunia, ulioandamwa na hofu ya Amerika kupoteza ushawishi wake wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Ni makosa kwa IG Koome kujibizana na wanasiasa

Wahudumu wa afya kaunti 12 watoa ilani ya kuanza mgomo

T L