• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
WANDERI KAMAU: Rais amjaribu Nelson Marwa kukabili majangili Bondeni

WANDERI KAMAU: Rais amjaribu Nelson Marwa kukabili majangili Bondeni

NA WANDERI KAMAU

WAKATI matatizo yanapomzidia mwanadamu, ni bora kumtafuta mtu, watu ama taasisi yenye uwezo wa kutatua changamoto hizo.

Hata hivyo, mkasa uliopo katika maisha ya mwanadamu ni kuwa hata wakati anapokumbwa na changamoto, huwa anatumia njia za mkato kutafuta suluhisho la changamoto hizo.

Ni jambo lisilowezekana. Ni juhudi ambazo kamwe haziwezi kuzaa matunda.

Urejeleo huu mfupi unatokana na hali ya ukosefu wa usalama inayoendelea kuikumba nchi, hasa katika maeneo ya ukanda wa Bonde la Ufa.
Ukweli ni kuwa, serikali inaonekana kushindwa na kudhibiti uhalifu unaoendelea kutekelezwa na majangili katika kaunti kama Baringo, Pokot Magharibi, Samburu, Laikipia, Turkana kati ya nyingine.

Kwa sasa, serikali hata imewatuma wanajeshi kukabiliana na majangili hao, lakini hali bado ni tete.

Majangili hao wanaonekana kutotishika hata kidogo. Licha ya uwepo wa majeshi, bado wanaendelea kutekeleza mashambulio yao dhidi ya wakazi wa kaunti hizo bila hofu zozote.

Kando na kutumwa kwa vikosi vya usalama, viongozi wakuu serikalini—akiwemo Rais William Ruto—wamenukuliwa wakitoa maonyo makali dhidi ya majangili hao.
Rais Ruto aliingilia kati baada ya maonyo ya Waziri wa Usalama, Kithure Kindiki, kutoonekana kuwatisha na kuwatikisa majangili hao. Mwelekeo huo bila shaka unaashiria kuwa tunafaa kuchukua hatua mpya kama nchi.

Moja ya hatua hiyo ni uteuzi wa Waziri mpya wa Usalama wa Ndani. Ukweli mchungu ni kuwa Prof Kindiki ameshindwa kabisa kuwakabili wahalifu hao.
Ijapokuwa uteuzi wake ulitokana na mchango muhimu aliotekeleza katika kampeni za Dkt Ruto alipokuwa akiwania urais mwaka uliopita, ni wakati Rais amteue mtu mwingine kuiongoza wizara hiyo, kwa kuzingatia uwezo wake wala si uzalendo wa kisiasa.

Tangu uhuru, teuzi zilizofanywa na marais wa hapo awali katika wizara hiyo zilihusisha watu wenye uwezo mkubwa kukabili ukosefu wa usalama au magenge ya uhalifu yanayochipuka, hasa nyakati za chaguzi kuu.

Licha ya makosa waliyohusishwa nayo, marais kama Mzee Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Uhuru Kenyatta walizingatia uwezo wa watu waliowateua kuhudumu katika nyadhifa hizo, badala ya uzalendo au ukaribu wa kisiasa uliokuwepo baina yao na watu hao.

Baadhi ya mawaziri wanaosifika sana kwa utendakazi wao ni marehemu John Michuki, Profesa George Saitoti na Dkt Fred Matiang’i, kwani walifaulu kukabili magenge ya uhalifu na wizi wa mifugo katika maeneo ya Bonde la Ufa.

Kwa kuzingatia mwelekeo wa watangulizi wake, tunampendekezea Rais Ruto angaa kumteua aliyekuwa Mshirikishi Mkuu wa Ukanda wa Pwani, Nelson Marwa, kuchukua nafasi ya Prof Kindiki kutokana na mchango aliotoa katika kukabiliana na ugaidi alipohudumu kama Kamishna wa Kaunti ya Mombasa.

Ukweli ni kuwa, utendakazi wa Bw Marwa kukabili ugaidi jijini Mombasa na eneo la Pwani kwa jumla unamfanya kuwa mtu bora zaidi kuhudumu katika nafasi hiyo.
Ili kuwashinda majangili Bondeni, pengine Bw Marwa ndiye tiba tunayohitaji.

  • Tags

You can share this post!

Ikulu ndogo jijini Mombasa hatarini kuporomoka

TAHARIRI: Serikali ifichue mashirika yaliyopigwa marufuku...

T L