• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
WANDERI KAMAU: Sauti za jamii ndogo zianze kusikika katika uongozi

WANDERI KAMAU: Sauti za jamii ndogo zianze kusikika katika uongozi

NA WANDERI KAMAU

JE, ni lini tutazikumbuka jamii ndogo nchini?

Ni lini watu wachache watapata usemi wao katika jamii? Ni lini mchango wao utatambulika?

Sababu kuu ya kuzua maswali hayo ni kuwa tangu tulipojinyakulia uhuru, ni jamii chache pekee—zinazosawiriwa kuwa ‘kubwa’— ndizo zimekuwa zikidhibiti karibu kila sekta muhimu nchini.

Ni taswira ambayo imeifanya Kenya kuonekana kama taifa la jamii chache tu, huku nyingine zikiwa kama maskwota au wakimbizi katika nchi yao wenyewe.

Ni hali ambayo imezinyima sauti kabisa jamii hizo. Hazisikiki wala kutambulika hata kidogo.

Nazungumzia jamii kama Elmolo, Yaaku, Bongo, Ogiek na Bongomek kati ya nyingine.

Kulingana na takwimu za Sensa ya 2019, idadi ya watu kutoka jamii hizi ni chache sana.

Kwa mfano, Waelmolo (wanaoishi karibu na fuo za Ziwa Turkana) ni chini ya watu 5,000.

Hata hivyo, idadi hiyo ni ongezeko kubwa kwani katika miaka ya 1970, jamii hiyo ilikuwa na chini ya watu 500.

Ijapokuwa katika uhalisia wa kisiasa ni kuwa jamii hupata nguvu kulingana na idadi yake, hiyo si sababu mahsusi hata kidogo ya kuzibagua na kuzitenga jamii hizo katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na uongozi wa nchi.

Kote duniani, kuna mifano ya nchi na falme nyingi zinazoongozwa na viongozi ambao hawatoki katika jamii kubwa zilizo katika nchi ama falme husika.

Kwa mfano, ijapokuwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameligeuza taifa hilo kuwa mali yake binafsi, yeye anatoka katika jamii ya Banyankole—ambao si wengi, ikilinganishwa na jamii kubwa kama Baganda au Bagisu.

Hapa Kenya, Rais Mstaafu (marehemu) Daniel arap Moi alitoka katika jamii ya Watugen, ambayo ni moja ya jamii ndogo miongoni mwa Wakalenjin. Kama Rais Museveni, hii ni licha ya maovu aliyotenda.

Ijapokuwa mwelekeo huu haumaanishi kuwa kiongozi kutoka jamii ndogo hawezi kufanya maovu, msimamo wa makala haya ni kuwa ni wakati mwafaka kwa jamii hizo kupewa nafasi ya kutoka katika uongozi wa nchi zao.

Hapa Kenya, imekuwa kawaida kwamba jamii tano ‘kubwa’ —zinazojumuisha Agikuyu, Wakalenjin, Abaluhya, Akamba na Waluo—ndizo zimekuwa zikishikilia idadi kubwa ya nafasi katika mashirika ya serikali.

Hilo lilidhihirishwa na ripoti iliyowasilishwa juzi kwa Kamati ya Bunge kuhusu Utangamano na Mshikamano wa Kitaifa.

Kulingana na ripoti hiyo, jamii za Agikuyu na Wakalenjin ndizo zinazoongoza kwa kushikilia nafasi nyingi zaidi katika mashirika ya serikali.

Bila shaka, huu si mwelekeo wa kuridhisha hata kidogo, hasa ikizingatiwa kuwa Rais na Naibu Rais wanatoka katika jamii hizo.

Kile tunachofaa kuanzisha kwa sasa ni mkakati wa kuondoa dhana ya Kenya kuonekana kama taifa la jamii mbili au tano pekee.

Ni mkakati unaofaa kukumbatiwa na mashirika yote ya serikali na sekta ya kibinafsi ili kuhakikisha kuwa tumejenga mazingira yatakayozitambua jamii ndogo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kenya Kwanza wamtongoza Shahbal

Kisasi: Waliopinga KK waanza kukiona

T L