NA WANDERI KAMAU
UTAKUMBUKWA vipi ukiondoka katika dunia hii?
Utakumbukwa kwa mateso uliyowaelekezea wenzako au wema uliowatendea?
Utakumbukwa kwa kujipenda au kutumia mali uliyo nayo kuwasaidia wasiojiweza? Utakumbukwa kwa kutumia kipaji alichokupa Mungu kujifaidi mwenyewe au wengine? Ungetaka jina lako likumbukwe vipi?
Haya ni baadhi ya maswali tunayopaswa kujiuliza tunapoendelea kuishi katika dunia hii kila siku, kwani ukweli mchungu uliopo kuhusu maisha ya mwanadamu ni kuwa, siku moja ataondoka na kumrudia Muumba.
Ingawa maisha ya mwanadamu si marefu sana—ikizingatiwa anaishi wastani wa miaka 70—amepewa uwezo wa kipekee na Mwenyezi Mungu.
Kinyume na viumbe wengine, mwanadamu amepewa uwezo mkubwa wa kiakili anaoweza kutumia kuboresha maisha yake binafsi ya uumba wake Mwenyezi Mungu.
Hata hivyo, kile husikitisha ni kuwa licha ya ufahamu huo wote, mwanadamu amekuwa akiishi maisha ya kutojali. Huwa hajali hata kidogo, kwa mfano, kuhusu vile atakavyokumbukwa akifariki, sifa atakayoacha duniani na [pengine] jinsi atakavyopokelewa katika ‘dunia mpya’ atakayoelekea baada ya kuondoka hapa ulimwenguni.
Katika historia, kuna mifano ya watu wengi wanaoendelea kukumbukwa kutokana na michango waliyotoa katika kuboresha maisha ya wanadamu wenzao.
Vivyo hivyo, kuna watu wengi wanaokumbukwa kwa kutumia nafasi na uwezo waliokuwa nao kuvuruga maisha ya wanadamu wenzao.
Baadhi ya watu wanaokumbukwa kwa kutumia nafasi waliyokuwa nayo kuwafaa binadamu wenzao ni Mother Teresa of Calcutta (wa Kanisa Katoliki), mwanaharakati Martin Luther King, mwanaharakati wa Weusi Rosa Parks, Papa John Paul II, Karolo Lwanga (aliyeuawa nchini Uganda na Kabaka Mwanga), muuguzi Florence Nightingale kati ya wengine wengi.
Hawa ni watu waliotumia ushawishi waliokuwa nao kuwafaa mamilioni ya watu waliohitaji usaidizi wao—si wa kifedha au kiraslimali tu—bali wa ukombozi wa kisiasa, kijamii, kiuchumi na kielimu.
Pia, kuna watu wanaokumbukwa kwa ukatili waliowatendea binadamu wenzao. Waliwadhuru mamilioni ya watu kwa kukiuka taratibu za kiutendakazi walizopaswa kuzingatia walipochukua nafasi hizo.
Ingawa sisi si Mungu kuwahukumu kulingana na vitendo vyao (kwani huwa tunakosea pia), ukweli uliopo ni kuwa vitendo vyao viliwaathiri wanadamu wengi.
Kwa mfano, Hitler analaumiwa kwa mauaji ya kikatili ya zaidi ya Wayahudi milioni sita kote ulimwenguni, hasa barani Ulaya.
Alipozikwa Jumamosi nyumbani kwake katika eneo la Gem, Kaunti ya Siaya, ni wazi kuwa sifa aliyokumbukwa nayo marehemu Profesa George Magoha ni mchango wake mkubwa aliotoa katika sekta ya elimu.
Nilipotazama hafla hiyo na kuona hotuba mbalimbali zikitolewa kuhusu utendakazi na mchango wake mahsusi, swali lililonijia akilini ni: Je, sisi tutakumbukwa vipi tukifariki?
Jibu lipo nasi sisi wenyewe. Ni wakati tuanze kupalilia maisha yetu tukiwa bado hai kabla ya siku yetu ya mauti kufika.