Maonyesho ya kilimo na biashara yanoga jijini Nairobi

Maonyesho ya kilimo na biashara yanoga jijini Nairobi

NA SAMMY WAWERU

MAONYESHO ya Kimataifa ya Kilimo na Kibiashara jijini Nairobi yameingia siku yake ya nne leo, Alhamisi.

Shoo hiyo inayoandaliwa kila mwaka na Muungano wa Kilimo Nchini (ASK), ilianza Jumatatu, Septemba 26.

Inafanyika katika uwanja wa Maonyesho wa Jamhuri Park.

Hafla hiyo aidha inaendelea hadi Jumapili, Oktoba 2 wakulima wakipata fursa ya mafunzo kuendeleza kilimo cha kisasa.

Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua alizindua rasmi shoo hiyo jana akiahidi kwamba serikali mpya ya Kenya Kwanza imeweka mikakati maalum kuboresha sekta ya kilimo na biashara.

Bw Gachagua alitaja mpango wa mbolea ya bei nafuu kama mojawapo ya mikakati kusaidia kupunguza gharama ya chakula nchini.

Wiki iliyopita, serikali ilizindua usambazaji wa mifuko 1.4 milioni ya fatalaiza chini mpango wa ruzuku ya mbolea, kufuatia ahadi ya Rais William Ruto wakati akiapishwa.

“Tunataka bidhaa zetu za kilimo na biashara ziwe na ushindani mkuu katika masoko ya ng’ambo,” akasema Naibu wa Rais, akihutubu wakati wa uzinduzi rasmi.

Bw Gachagua aidha alitumia jukwaa la maonyesho hayo kutangaza kwamba mabalozi na maafisa watakaoteuliwa kuwakilisha Kenya mataifa ya nje, watalazimika kutia saini mkataba wa makubaliano kusaka mianya ya soko ya mazao ya kilimo.

“Kila baada ya miaka miwili, tutakuwa tunatathmini utendakazi wao kubaini ikiwa wametuletea wanunuzi,” akasema.

Naibu Rais vilevile alitangaza kwamba serikali imetenga kima cha Sh3 bilioni, kugharamia bima ya hasara ya mimea inayotokana na ukame, mkurupuko wa magonjwa na wadudu.

Naibu Rais Rigathi Gachagua wakati wa ufunguzi rasmi Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo na Kibiashara Jijini Nairobi (ASK), Jamhuri Park Showground Jumatano. PICHA | SAMMY WAWERU

Mpango huo utashirikisha wakulima milioni 1.3 katika kaunti 37.

Shoo ya Nairobi ASK makala ya 120, mifumo ya kisasa kuboresha shughuli ya kilimo ni miongoni mwa teknolojia na bunifu zinazoonyeshwa.

Mada ya mwaka huu ikiwa, ‘Kuboresha Kilimo na Biashara kupitia Teknolojia na Ubunifu’, kero ya tabianchi imepewa kipau mbele wakulima wakihimizwa kukumbatia teknolojia za kisasa kuendeleza zaraa.

Jumla ya waonyeshaji 350, 300 wakiwa wa humu nchini na 50 kutoka ng’ambo wanashiriki.

Wamekusanywa kutoka mtandao na utandawazi wa kilimo, viwanda, makazi, wafanyabiashara wa mapato ya kadri na ya chini (SMEs), teknolojia, uvumbuzi, mashirika ya kifedha, sekta ya umma na kininafsi, na utalii.

Hafla ya mwaka huu, kulingana na Waziri Msaidizi Wizara ya Kilimo (CAS), Anne Nyaga inajumuisha wanafunzi chini ya mpango wa 4 K Club kuonyesha umahiri wao katika kilimo.

Imerejea miaka miwili, baada ya kusitishwa na mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini.

“Virusi vya corona vilirejesha nyuma sekta ya kilimo. Maonyesho kama haya ni mojawapo ya majukwaa kusambaza jumbe na ushauri kwa wakulima,” Bi Anne akasema..

Ada ya kuingia ni Sh250 kwa watoto na wanafunzi kila mmoja, na Sh300 watu wazima.

  • Tags

You can share this post!

Putin ataja maeneo 4 Ukraine kuwa ya Urusi

Lionel Messi afunga mabao mawili na kusaidia Argentina...

T L