Habari Mseto

Mapadre, watawa na waumini 46 wakamatwa kwa kusali kinyume cha sheria

March 28th, 2020 1 min read

BRIAN OJAMAA NA FAUSTINE NGILA

Polisi Jumamosi waliwatia baroni makasisi wawili, watawa kadhaa na waumini 46 waliokuwa wakisali katika makanisa mawili ya Katoliki Bungoma.

Walikamatwa kwa kuwa walikaidi amri ya serikali inayopiga marufuku mikusanyiko yoyote, ili kupambana na janga la virusi vya corona.

Waumini 34 walikamatwa katika kanisa la katoliki la Christ the King na wengine 14  katika kanisa la St Paul’s Kanduyi.

Kizaazaa kilishuudiwa wakati wafuasi waliamua kutimua mbio huku polisi ambao hawakuwa wamevalia sare walifika katika makanisa hayo kuwanasa.

Naibu kamshina katika eneo la Bungoma Kusini  Bw Michael Yator alisema waumini hao walizuiliwa kwa muda mfupi kisha wakaachiliwa huru.

“Tuliwaachilia baada ya kuwaonya kuwa hakuna mikusanyiko inayokubaliwa na kila mtu anapaswa kuombea nyumbani,” alisema.

Naibu mshirikishi wa Kanduyi Bw Abdi Shakur aliwataka watakatifu kufuata amri ya serikali ya kutohudhuria mikutano yeyote.

“Tunawahimiza watu wote waepuke mikutano ya makasina, masoko, misikiti, vilabu na mikutano mingine yoyote ili kusaidia kuzuia kusambaa kwa virusi vya korona,” alisema.