Makala

Mapato duni, elimu finyu vyatajwa kuwa vichocheo vya dhuluma dhidi ya wanawake

Na LEAH MAKENA August 14th, 2024 1 min read

Sababu zinazohusishwa na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake

Ukatili dhidi ya wanawake haswa walio kwenye ndoa ni moja ya mambo makuu yanayowasababishia matatizo ya kiafya.

Kulingana na utafiti wa shirika la afya duniani WHO, asilimia 30 ya wanawake duniani wamewahi kupitia ukatili wa kijinsia au wa kimwili kutoka kwa wapenzi wao au waume wa kawaida katika maisha yao.

Ukatili huu unaweza kuathiri wanawake kiakili, kimwili, kingono, kiuzazi au hata kuwaweka katika hatari ya kuambukizwa virusi vya ukimwi.

Mojawapo ya mambo yanayosababisha ukatili dhidi ya wanawake ni ukosefu wa elimu kuhusu hatari ya vurugu nyumbani. Baadhi ya wanaume wanakosa ufahamu wa jinsi ya kukomesha unyanyasaji dhidi ya wake zao.

Sababu nyingine ni matumizi ya dawa za kulevya. Ulevi hufanya wakatili kuzua vurugu bila kujali matokeo hasi ya vitendo vyao.

Pia, tamaduni nyingi zinazodunisha jinsia ya kike zinawapa wanaume mamlaka ya kufanyia wanawake chochote bila kujali kwa sababu hakuna wa kuwachukulia hatua.

Mbali na hayo, wanawake ambao hawana kipato na husalia kutegemea waume zao kwa kila jambo ambapo hujipata wakinyanyasika na huwa hawana uwezo wa kujitetea wanapotendewa ukatili wa aina yoyote.

Aidha, wanandoa ambao wamekua kwenye mazingira ya vita na vurugu huchukulia suala la ukatili kama jambo la kawaida. Hivyo basi, wanawake husalia kimya wanaponyanyaswa kwa sababu hudhania ni desturi.

Kando na sheria zilizoundwa za kulinda wanawake dhidi ya unyanyasaji, ni muhimu kuunda sera zinazokuza usawa wa kijinsia, kufanya mikakati itakazowezesha wanawake kujisimamia kifedha na kuweka kanuni zitakazolinda haki zao.