Habari Mseto

Mapato ya maua, mboga na matunda yaongezeka

February 13th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Mapato kutokana na kilimo cha maua, mboga na matunda yanaendelea kuimarika. Katika ripoti ya hivi punde kuhusiana mapato nchini, kilimo hicho ni cha tatu kuipa Kenya mapato mengi zaidi kutoka biashara ya kimataifa.

Ongezeko la mapato kutokana na mauzo ya maua, matunda na mboga lilikuwa asilimia 33 kutoka Sh115 bilioni mwaka mmoja uliokuwa umetangulia.

Ongezeko hilo lilitokana na ongezeko la mahitaji na pia bei ya mauzo katika soko la kimataifa. Mwaka jana, biashara hiyo iliipa Kenya Sh153 bilioni.

Maua ndio yalitoa mapato mengi zaidi (Sh113 bilioni) ambapo mboga iliipa Kenya Sh27 bilioni na matunda Sh12 bilioni.

Hata hivyo, wananchi wanaoishi nje ya nchi bado wanaongoza kwa kiwango cha mapato ya kimataifa baada ya kuipa Kenya Sh272 bilioni na kufuatwa na utalii ambapo Kenya ilipata Sh157 bilioni.