KAULI YA MATUNDURA: Mapema mno kusherehekea mchakato wa kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili la Kenya

KAULI YA MATUNDURA: Mapema mno kusherehekea mchakato wa kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili la Kenya

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA kipindi cha mwezi mmoja uliopita, matukio matatu yalizua msisimko katika ulimwengu wa Kiswahili.

Kwanza, gazeti la Taifa Leo lilizinduliwa upya.

Pili, Shirika la Umoja wa Mataifa, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lilitangaza kuwa Julai 7 itakuwa Siku ya Kiswahili Duniani kila mwaka.

Tatu, Kamati ya Idara ya Michezo, Utamaduni na Utalii Bungeni iliwasilisha hoja Bungeni, kuhusu kubuniwa kwa Baraza la Kitaifa la Kiswahili la Kenya (BAKIKE).

Hatua hizi hazipaswi kupingwa – bali kuungwa mkono.

Hata hivyo, ni mapema mno kwa mfano, kuanza kusherehekea kufufuliwa kwa mchakato wa kubuniwa kwa BAKIKE kwa sababu zifuatazo.

Kwanza, huu ni mchakato wa kisiasa na wanasiasa huenda wasifahamu dharura ya Kenya kuwa na asasi hii.

Pili, wataalamu wa Kiswahili hawapaswi kukaa pembezoni na kusubiri wanasiasa waendeshe mchakato huu.

Kuna haja ya vyombo kama vile Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) kufanya mikakati na kampeni za chini kwa chini kuongeza kani itakayochapusha mchakato huo.

Ilivyo ni kwamba, Kenya imechelewa mno katika kuwa na Baraza la Kiswahili.

Kuchelewa huku ama ni kwa kimakusudi – au waliotwikwa jukumu la kuhakikisha Baraza hili linabuniwa ama wamezembea katika kazi yao au hawaoni umuhimu walo.

Wadau wa Kiswahili wanapaswa kushinikiza mchakato huu uwe na makataa ya kukamilishwa.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Ali Salim M’Manga

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kukuza na kuendeleza Kiswahili...

T L