Habari Mseto

Mapendekezo ya kulainisha sekta ya kahawa

December 20th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKULIMA wa kahawa watapata afueni baada ya kuwekwa mapendekezo ya kulainisha sekta hiyo.

Mnamo Jumamosi Waziri wa Kilimo Bw Peter Munya alizuru eneo la Gathage, Gatundu Kusini kwa lengo la kuwasomea mapendekezo mapya ya kulainisha sekta ya kilimo cha kahawa.

Zaidi ya wakulima 1,000 walihudhuria hafla hiyo ili kupata mawaidha kuhusu mambo mapya yaliyomo katika mkakati wa kuboresha sekta ya kahawa.

Waziri alisema mkulima wa kahawa atakuwa na sauti kubwa katika uamuzi wa mauzo ya zao hilo katika soko la mnada au oksheni.

Alisema maswala mengi yataendeshwa kwa njia ya kidijitali ili kuharakisha mambo.

Pendekezo lingine ni kwamba viwanda vyote vilivyofungwa vitafunguliwa upya ili kuwapa wakulima nafasi ya kurejelea kilimo hicho.

Halmashauri ya New KPCU itakuwa mstari wa mbele kuwasaidia wakulima kunufaika na kahawa yao.

“Wakati huu tumeamua kuwa hakuna mkulima atapunjwa kutokana na kahawa yake kwani tunaelewa kahawa nyingi huwa ni za gredi ya juu. Lakini mawakala ndio wamekuwa kikwazo cha kufanya mambo kuwa magumu kwa mkulima,” alisema Bw Munya.

Baada ya kusoma pendekezo la sheria mpya iyakayowasilishwa bungeni, wakulima kwa kauli moja waliipitisha bila pingamizi yoyote.

Baadhi ya mapendekezo aliyosomea wakulima hao ni kwamba kituo cha utafiti kitazinduliwa upya.

Pia kutakuwa na soko wazi ambapo mtu yeyote ana ruhusa ya kununua kahawa na kuiuza kwingineko jinsi apendavyo.

Wasagaji kahawa hawataruhusiwa kukopesha pesa kwa vyama vya ushirika kama hapo awali.

Kabla ya jambo lolote kutendwa kuhusu mali ya wakulima ni sharti kuwepo na kikao na maelewano miongoni mwa wakulima.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya New KPCU Bw Henry Kinyua alisema afisi yake iko tayari wakati wowote kuwasaidia wakulima kusaga kahawa yao na kutafuta soko la nje.

“Sisi tutaendelea kushirikiana vyema na wakulima wa kahawa ili waweze kufurahia jasho lao. Tunaelewa wamepunjwa kwa muda mrefu,” alisema Bw Kinyua.

Alisema mkulima atakuwa na uhuru wake wa kuelewana na mnunuzi hata kupitia njia za mtandaoni ili kupata haki yake kamili.

“Baada ya wakulima kupitia shida nyingi kutokana na zao hilo sasa mambo yatakuwa shwari kwao kwani wao ndio wenye mali,” alisema Bw Kinyua.