Makala

MAPENZI MITANDAONI: Wengi wanasaka uroda, wengine ni mashoga ila kuna wenye nia njema

March 12th, 2020 2 min read

NA WEMA KAIMENYI 

Je, unaweza kumwamini mpenzi unayempata mtandaoni? Je, unaziamini picha za watu uwapatao mtandaoni? Mapenzi ya mtandaoni yana uwezo wa kustahimili?

Beatrice, 20, ambaye ni mwanfunzi wa chuo kikuu anasema hakubaliani kamwe na mapenzi haya.

“Mwaka jana karibu niyapoteze maisha yangu kwa sababu ya mwanaume niliyempata Instagram, tukaongea kwa muda na hatimaye tukakubaliana nimtembelee baada ya kunitumia nauli. Nilipofika kwake, Jack alinipokea vizuri na kuninunulia vinywaji.

“Usiku ulipowadia , nilitaka kuondoka lakini alikataa na akanishawishi nikae naye ili nisafiri siku iliyofuata,” anaeleza.

Baada ya giza kuingia, alitaka washiriki ngono, ila Baetrice alikataa kwa kuhofia kuambukizwa Ukimwi.

“Ghafla bin vuu, Jack aligeuka kuwa mnyama. Alinizaba makofi na kunitema nje usiku. Nilijuta kwa kuamini picha tu ya mtandaoni. Kumbe picha haiwezi kueleza sifa kamili za mtu,” aliambia Taifa Leo Dijitali.  

Kelvin, 27, ambaye ni mkazi mjini Eldoret anasema kuwa ingawa wengi wetu hawana imani na mapenzi ya mtandaoni, si kila mtu unayempata pale ana nia mbaya.

“Mpenzi wangu Lucy, mama ya mtoto wangu , nilimpata pale Facebook. Tulipopanga kukutana, nilikuwa na uoga lakini ile haja ya kumpata mchumba ilinisukuma. Baadaye tulikutana pale City Gardens. Na kusema ukweli alinipendeza,” anafichua.

Kevin alipohojiwa na Taifa Leo Dijitali. Picha/ Wema Kaimenyi.

Wazazi wake walimuonya dhidi ya uhusiano huo mara ya kwanza, lakini baadaye walikubali. Miaka mitatu baadaye walifunga pingu za maisha .

“Kwa hivyo, binadamu umpate mtandaoni ama kwa maisha ya kawaida atabaki kuwa binadamu tu. Na anaweza kubadilisha nia wakati wowote,” anasema.

Lakini Gideon, 23, pia mwanafunzi, anasema kuwa kumwamini mtu umpataye mtandaoni ni ubaradhuli wa hali ya juu kwani watu wa mtandaoni wanatumia majina na picha bandia zisizoweza kuaminika.

“Miaka miwili iliyopita, nilimtamani mwanadada pale Facebook na sikuwa na budi ila kumweleza nia yangu ya kimapenzi naye. Siku ya siku ilifika, siku ambayo tuliagana kupatana katika hoteli moja. Nililipia chumba na kumwelekeza atakaponipata. Baada ya muda, mlango ulibishwa na kwa hamu kubwa nikamwomba aingie,” anaeleza.

Gideon alishangaa kuwa wapo wanaume mitandaoni wanaoweka picha za mabinti kuvutia wanaume. Picha/ Wema Kaimenyi

Hata hivyo, aliduwaa alipong’amua kuwa aliyemwita aje chumbani si binti bali janadume kama yeye.

“Nilishtuka alipoingia mwanamume mwenzangu na kuketi kando yangu. Alinieleza kuwa yeye ndiye mgeni wangu. Mungu wangu! Kijasho chembamba kilianza kunitiririka. Nikamweleza kuwa nilikua namtarajia mwanadada,” anasema.

Mwanamume huyo alimweleza Gideon kuwa yeye hushiriki na wanaume wenzake , jambo ambalo lilifanya Gideon kuchana mbuga kutoka chumbani humo na kuisahau simu yake.