Bambika

Mapenzi yamlemea maskini Mondi akitangaza yuko singo

January 19th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

YAONEKANA mwanamuziki staa wa Bongo flava Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz ana mlima wa kukwea likija suala la mapenzi.

Licha ya uvumi kuenea kila pembe ya dunia kwamba mmiliki huyo wa lebo ya Wasafi anatoka kimapenzi na msanii wake Zuhura Othman almaarufu Zuchu, chapisho lake la Jumatano kwa Instagram limeonyesha vinginevyo.

Mondi, kama anavyofahamika na wengi, sasa ametangaza kwamba yuko singo.

“Kuanzia leo ningependa niwatangaze rasmi kuwa I AM SINGLE, sichumbii wala sina mahusiano na mwanamke yeyote,” akasema Diamond.

Kwenye chapisho hilo katika mtandao wa Instagram, baba huyo wa watoto watano aliwasihi mashabiki wake kuacha kumpa mpenzi yeyote. Alisema akimpata mpenzi atatangaza rasmi.

Sasa yaonekana kwamba mabusu yake na Zuchu yalikuwa ni kazi bure!

Chapisho hilo lake linakuja baada ya mamake Bi Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote, kutoa kauli hadharani kuwa Zuchu hatambuliki kuwa mkaza mwanawe.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Wasafi Media, Mama Dangote alibainisha kuwa mwanawe ambaye ni bosi huyo wa WCB, hajawahi kumtambulisha Zuchu kama mpenzi wake.

“Diamond hajawahi niletea Zuchu eti anataka kumuoa. Mimi kwanza najua Zuchu ni msanii wake,” akasema Mama Dangote.

Akaongeza: “Kusema eti Zuchu ni mchumba wake sijui kwa sababu mimi sijapeleka mahari kwa kina Zuchu wala barua. Zuchu namjua ni msanii wake. Kila siku tuko naye sijui. Najua ni msanii.”

Kwenye mahojiano hayo, Mama Dangote alibainisha kuwa Zuchu si mwanamke wa kwanza kuhusishwa kwamba anatoka kimapenzi na mwanawe kwani amekuwa akidaiwa kutoka na wanawake wengine wengi waliowahi kuonekana naye katika siku za nyuma.

Kwa muda mrefu, Diamond na Zuchu wamekuwa wakidaiwa kuwa wapenzi na mara nyingi wamekuwa wakionekana wakishiriki hafla kama bethidei kwa mapozi ya kichokozi na kupigana mabusu mbele ya mashabiki wao.

Mwaka 2023, malkia wa Taarab Khadija Kopa ambaye ni mamake Zuchu, pia alikana kuwepo kwa uhusiano wa kimapenzi kati ya mwanawe na bosi wake.