Makala

MAPISHI: Biriani ya nyama ya mbuzi

September 4th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kuandaa: Dakika 20

Mapishi: Dakika 40

Walaji: 3

Biriani ni chakula kinachotengenezwa kwa wali uliokaangwa na kuchanganywa na nyama ambayo imekaangwa na masala.

Vinavyohitajika

 • mchele wa Basmati nusu kilo
 • kilo moja ya nyama ya mbuzi (kata katika umbo dogo kisha ichemshe pamoja na tangawizi, kitunguu saumu, unga wa binzari, pilipili na chumvi)
 • vitunguu maji vinne
 • nyanya sita (kata vipande vidogovidogo)
 • mafuta ya kupikia
 • kijiko kimoja kidogo cha pilipili
 • unga wa binzari nusu kijiko
 • vijiko vitatu vya unga wa giligilani
 • vijiko viwili vya mchanganyiko wa tangawizi na kitunguu saumu (vya kusagwa)
 • mbegu 10 za hiliki au iliki (green cardamoms)
 • majani manne ya bay
 • majani ya mint
 • chumvi kulingana na mahitaji yako

Maelekezo

Mimina mafuta katika sufuria yapate moto kisha kaanga nyama yako iliyokwisha chemshwa mpaka iwe na rangi ya kahawia.

Ikishaiva, itoe nyama hiyo na ichuje mafuta na mafuta yanayobaki weka kitunguu na endelea kukaanga kwa dakika 10 kisha weka binzari, pilipili, giligilani, bay leaves na mbegu za hiliki.

Changanya vizuri upate mchanganyiko mzuri mkavu, halafu mwagilia yale maji ‘uliyotunza’ baada ya kuchemsha ile nyama yako

Sasa weka nyanya ndani ya sufuria yako na upike mpaka maji yakauke na mafuta yaanze kuoneka kwa juu ndani ya sufuria.

Weka nyama yako ndani ya sufuria halafu punguza moto ili ipikike kwa muda mpaka mchuzi wako na nyama viwe na ladha. Pia usisahau kuongeza chumvi kulingana na ladha unayopenda.

Chukua sufuria nyingine, mimina mafuta ya kupikia na vitunguu kisha kaanga na majani ya giligilani, majani ya mint na korosho kisha funika kwa dakika 10.

Weka mchele wako mkavu uliokwisha oshwa vizuri na uchanganye vizuri. Ongeza vikombe vitano vya maji na chumvi kiasi.

Mchele ukishaanza kuchemka, funika sufuria yako na punguza moto. Maji yakishakauka kiasi, weka mchanganyiko wa ile nyama yako nusu tu juu ya wali wa Basmati na acha wali uive kabisa.

Ni muda mchache tu halafu utakuwa tayari mlaji kupakua na kula chakula kabla hakijapoa sana.

Kikishakuwa tayari, pakua na ufurahie.