Makala

MAPISHI: Jinsi ya kuandaa vipapatio vya kuku vyenye asali

July 23rd, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kuandaa: Dakika 20

Muda wa kupika: Dakika 40

Walaji: 4

Vinavyohitajika

  • Kilo 1 ya vipapatio vya kuku
  • Vitunguu saumu 4, menya kisha saga
  • Vijiko 3 vya asali
  • Kijiko 1 cha soy sauce
  • Kijiko 1 cha pilipili ya unga
  • Mafuta ya kupikia
  • Juisi ya limau
  • Chumvi

Maelekezo

Anza kwa kuviandaa vipapatio vya kuku. Vioshe vizuri kisha weka kwenye chombo kilicho safi.

Ongeza juisi ya limau, weka chumvi nusu kijiko na pilipili.

Koroga vizuri kwa mikono hadi zichanganyike vizuri. Hifadhi kwenye jokofu kwa muda wa saa mbili ili viungo vichanganyike na nyama ya kuku vizuri.

Vipande vya kuku vikiwa vimetiwa viungo. Picha/ Margaret Maina

Weka kikaangio chenye mafuta mekoni. Mafuta yakipata moto, weka kuku huku ukigeuza mara kwa mara.

Acha nyama ya kuku iive vizuri kisha toa na uhifadhi pembeni au kando.

Kwenye kikaangio tofauti, mimina mafuta ya kupikia kisha bandika kwenye meko yenye moto wa wastani.

Mafuta yakipata moto, weka kitunguu saumu. Koroga na acha kiive hadi kianze kubadilika rangi; kuwa makini uhakikishe hakiungui.

Weka asali, soy sauce, na pilipili. Koroga vizuri. Acha vichemke na kuchanganyika kwa muda wa dakika moja.

Weka vipapatio vya kuku, koroga vizuri zaidi. Ongeza moto ili asali na soy sauce vitoe povu kiasi, na kutoa hali au dalili ya kama kuungua na kunata.

Epua, pakua na ufurahie.