MAPISHI: Jinsi ya kupika katlesi tamu za samaki

MAPISHI: Jinsi ya kupika katlesi tamu za samaki

Na MARY WANGARI

Vinavyohitajika

 • samaki bila mifupa yaani fish fillets
 • 3 mayai
 • 8 viazi mbatata vikubwa
 • 2 karoti kubwa
 • 2 vitunguu maji vikubwa
 • 1 ndimu
 • 1 pilipili mboga kubwa
 • 1 iliki kubwa
 • 1 kijiko kikubwa cha bizari ya manjano
 • chenga za mkate
 • chumvi kiasi cha haja
 • mafuta ya kupikia

Utaratibu

Safisha samaki na ondoa mifupa kama ilikuwa imebaki. Weka samaki kwenye sufuria safi halafu ongeza maji kiasi na ubandike sufuria mekoni.

Ongeza tangawizi, kitunguu thomu, limau, funika na uiache itokote kwenye moto wa wastan hadi maji yakauke.

Menya viazi, safisha na uvikate mara mbili huku ukivitia katika karai safi.

Safisha karoti, pilipili hoho na uzikwangue, safisha kitunguu maji na ukatekate vipande vyembamba

Katika sufuria safi, weka viazi, tia maji, bandika mekoni halafu funika uviruhusu kutokota kwenye moto wa wastani.

Viazi vikishaiva, epua na umwage maji yaliyosalia.

Changanya nyama, viungo ulivyoandaa awali vya karoti, pilipili mboga na kitunguu maji kwenye viazi.

Ponda mchanganyiko wako hadi uvurugike na kushikamana vyema

Fanya madonge madonge yanaweza kuwa umbo la duara au duara dufu kwa raha zako.

Vunja mayai kwenye bakuli safi, koroga na uweke pembeni.

Chukua madonge uliyounda,,vigaragaze vyote kwenye chenga za mkate ulizotia kwenye sinia safi

Kwenye karai safi, mimina mafuta mengi kiasi ya kuchoma bandika mekoni na uache yashike moto.

Kisha chukua donge moja moja, chovya kwenye mayai, tumbukiza kwenye mafuta na kuchoma hadi yageuke rangi ya dhahabu hadi madonge yote yaishe.

Unapochoma katlesi zako, hakikisha mafuta yameshika moto kabisa na uepuke kuzigeuza geuza ili zisivurugike.

Mafuta yakiwa moto yatawezesha katlesi zako kuchomeka upesi na kuzuia zisivurugike kwa kukaa sana kwenye moto.

Epuka kugeuza geuza ili zisije zikavurugika kwenye mafuta, na mafuta yawe yamepata moto kiasi kwani zikikaa sana mekoni pia zinaweza kuvurugika.

Katlesi zako sasa zipo tayari kwa kuliwa na unaweza ukaambatisha kwa sharubati au vyovyote upendavyo.

Kando na samaki, unaweza pia ukatumia nyama ya ng’ombe iliyosagwa au nyama ya kuku uliyokata vipande vidogovidogo.

marya.wangari@gmail.com 

You can share this post!

Kongamano la ugatuzi kuhudhuriwa na wachache kutokana na...

Mtaalamu awaponda akina mama wanaodai wana maziwa kidogo