Makala

MAPISHI: Jinsi ya kupika minofu ya kuku yenye siagi

July 30th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa mapishi: Nusu saa

Walaji: 4

Vinavyohitajika

 • minofu au vipande vya kuku kilo 1
 • juisi ya limau
 • chumvi kijiko 1
 • pilipili ya unga vijiko 3
 • tangawizi iliyosagwa kijiko 1
 • majani ya bay 3
 • mdalasini uliosagwa kijiko 1
 • siagi vijiko 3
 • vitunguu maji 2
 • vitunguu saumu vijiko 5
 • giligiliani vijiko 2
 • nyanya ya kopo vijiko 2
 • maziwa mala vijiko 2
 • mafuta ya kupikia
 • chumvi

Maelekezo

Andaa nyama ya kuku; isafishe vizuri.

Chukua pilipili manga, tangawizi, majani ya bay, mdalasini, maziwa mala, vitunguu maji, vitunguu saumu, giligilani, na nyanya ya kopo. Chukua blenda weka hivyo vitu vyote kisha saga, hakikisha vimelainika kabisa na viungo vimechanganyikana vizuri.

Chukua kuku; kata mapande makubwa.

Chukua bakuli kubwa, weka hayo mapande kisha changanya na juisi ya limau halafu nyunyizia chumvi kiasi.

Mwagia mafuta ya kupikia kwenye kuku, changanya vizuri mpaka uone mafuta yameenea vizuri.

Chukua ile rojo mwagia kwenye kuku kisha changanya. Ukimaliza, weka kwenye jokofu kwa muda wa saa moja. Yatoe mapande ya kuku na upake siagi halafu changanya kabla ya kurudisha tena kwenye jokofu.

Acha mapande hayo usiku kucha.

Toa kuku ukaange na viungo upendavyo. Unaweza kuoka au kuchoma. Uamuzi ni wako.

Angalia saa. Dakika 25 zikifika, chakula kitakuwa kimeiva.

Pakua na chochote ukipendacho na ufurahie mlo!

Minofu ya kuku yenye siagi. Picha/ Margaret Maina