Makala

MAPISHI: Jinsi ya kupika onion rings

June 11th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

ONION rings ni kitafunwa kizuri kwa wale wanaoenda ziara nyanjani kujiburudisha – yaani picnic – au kwa watoto wanaoenda shule.

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa kupika: Dakika 20

Walaji: 4

Vinavyohitajika

  • Vitunguu maji 20
  • Unga wa ngano nusu kilo
  • Viini vya mayai 10 (tenganisha ute na kiini)
  • Chumvi kiasi cha kijiko kimoja
  • Maziwa kikombe kimoja
  • Mafuta ya kupikia
  • Mtindi (Sour cream)
  • Mayonnaise

Maelekezo

TAMBUA: Uko huru ama kuongeza au kupunguza viungo jinsi upendavyo.

Menya na kata vitunguu viwe umbo la duara kisha ziwe kama pete ila visiwe vipana sana maana huenda havitoiva vizuri.

Pasua mayai kisha tenganisha ute na kiini.

Changanya unga, viini vya mayai, maziwa, mafuta ya kupikia na chumvi.

Koroga pamoja hadi vichanganyike vizuri na uwe laini.

Changanya kidogokidogo ute wa yai kwenye mchanganyiko huku unakoroga.

Chovya vitunguu katika mchanganyiko wa unga. Hakikisha vimezama kabisa na uache vikae kwa muda kiasi.

Unaweza pia kuweka breadcumbs ili kuipa umbo pana zaidi.

Weka mafuta ya kupikia mekoni uache yapate moto vizuri kisha weka vitunguu vilivyopakwa ngano na kaanga kwa muda wa dakika 10.

Hakikisha mafuta yapo ya kutosha ili kila kitu kizame kwenye mafuta.

Toa vitunguu jikoni, weka kwenye karatasi (paper towel) ili kunyonya mafuta na kuziacha kavu.

Rudia shughuli hii kwa vitunguu vilivyobaki hadi viishe.

Pakua na ufurahie. Usisahau kuchanganya na sauce unayopenda – mayonnaise, ketchup au mtindi.