Makala

MAPISHI: Kuku wa masala na wali wa kuchemsha

March 5th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MCHANA huu tunaandaa nyama ya kuku iliyotiwa masala pamoja na wali wa kuchemsha.

Muda wa kuandaa: Dakika 15
Muda wa ku-marinate: Saa 2
Muda wa kupika: Dakika 20
Walaji: 4

Wali na nyama ya kuku na masala. Picha/ Margaret Maina

Vinavyohitajika kwa ajili ya kuku

 • Kuku 1
 • Nyanya 2
 • Vitunguu maji 2
 • Kijiko 1 cha tangawizi
 • Kijiko 1 cha kitunguu saumu
 • Limau 1
 • Pilipili
 • ½ kikombe maziwa ya mgando
 • Vijiko 6 vya mafuta ya kupikia
 • Majani ya kotimiri
 • Chumvi

Viungo

 • Majani 4 ya bay
 • Iliki
 • Mdalasini
 • Kijiko 1 cha garam masala
 • Vijiko 2 vya chicken bouillon powder
 • ½ kijiko cha coriander
 • ½ kijiko cha binzari ya pilau
 • ½ kijiko cha pilipili
 • ½ kijiko cha binzari ya manjano
 • Chumvi

Maelekezo

Osha, kausha na chanja kuku.

Gongagonga kitunguu saumu na tangawizi, kamua juisi ya limau na katakata majani ya giligilani.

Kwenye bakuli kubwa, weka minofu ya kuku, juisi ya limau, kijiko kimoja cha kitunguu saumu, kijiko kimoja cha tangawizi, chumvi, na vijiko viwili vya mafuta ya kupikia.

Changanya vizuri, funika na hifadhi kwenye jokofu kwa muda wa saa mbili.

Kwenye kikaango na katika moto wa juu, chemsha vijiko vitatu vya mafuta.

Tumbukiza kuku, kanga kila upande mpaka rangi ya ngozi iwe kahawia kiasi ila isikauke sana. Epua.

Weka nyanya, kitunguu na pilipili kwenye blenda.

Kwenye kikaango, chemsha mafuta kiasi cha kijiko kimoja. Ongeza viungo, vijiti vya mdalasini, iliki na bay leaf. Kaanga kwa sekunde kama 30 hivi.

Ongeza rojo ya nyanya, kitunguu na pilipili pamoja na viungo vilivyobakia; garam masala, chicken bouillon powder, binzari ya pilau, binzari ya manjano, coriander powder, na pilipili.

Ongeza mtindi, pika kiasi kisha ongeza kuku, na uchanganye vizuri.

Chakula hiki kikishaiva, pakua na ufurahie na wenzako; idadi yenu nyote isizidi watu wanne.