Makala

MAPISHI: Maini ya ng'ombe

May 22nd, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

MUDA wa kuandaa: Dakika 10

Muda wa kupika: Dakika 30

Walaji : 3

Maini ya ng’ombe kabla ya kupikwa. Picha/ Margaret Maina

Vinavyohitajika

 • Kilo 1  ya maini ya ng’ombe
 • Vijiko 4 vya mafuta ya kupikia
 • Kijiko 1 cha  tangawizi
 • Kijiko 1 cha kitunguu saumu
 • Pilipili mboga mchanganyiko nusu x3
 • Karoti 1
 • Nyanya 2
 • Kitunguu maji 1
 • Pilipili
 • Chumvi
 • Majani ya giligilani

 

Maini ya ng’ombe yakiwa yamepikwa. Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Weka nyanya na pilipili kwenye blenda utengeneze rojo.

Menya, osha na katakata maini.

Katakata kitunguu maji, pilipili mboga na karoti vipande vidogovidogo vya mraba.

Twanga kitunguu saumu na tangawizi kwenye kinu chako au kifaa kinginecho.

Katakata majani ya giligilani.

Kwenye sufuria katika moto wa wastani, weka mafuta.

Ongeza kitunguu maji, kitunguu saumu na tangawizi. Kaanga kwa dakika mbili.

Ongeza maini. Nyunyizia chumvi na uendelee kukaanga huku ukigeuzageuza hadi maini yapate rangi ya kahawia kiasi, ila yasiive kabisa.

Ongeza rojo ya nyanya na pilipili. Funika kisha acha kwa moto wa wastani mpaka nyanya ziive vizuri.

Ongeza karoti kisha weka pilipili mboga kwa dakika moja. Unaweza pia kuongeza maji kidogo kama unapenda mchuzi.

Pakua ule na tafuta chakula kingine cha kuungia; unaweza kula ugali.