Makala

MAPISHI: Mandazi

May 29th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa kupika: dakika 30

Walaji: 10

ANDAZI ni kitafunio ambacho unaweza ukakila hasa unapokuwa hapo nyumbani au kazini ukinywa chai, juisi au kinywaji chochote.

Unahitaji

  • Unga wa ngano kilo moja
  • Sukari vikombe viwili
  • Vanilla ya unga nusu kijiko cha chai
  • Chumvi nusu kijiko cha chai
  • Tui moja la nazi
  • Mafuta lita mbili

Maelekezo

Chemsha mafuta mpaka yachemke.

Weka unga kwenye bakuli au sufuria. Ongeza chumvi na kisha changanya. Chota mafuta kiasi cha vikombe viwili vya kahawa uyamimine kwenye unga.

Changanya vizuri kwa kutumia mwiko (tumia mwiko kwa sababu mafuta ni ya moto). Endelea kuchanganya kwa kutumia mikono kukanda mpaka unga uwe laini kabisa.

Ukishachanganyikana na mafuta vizuri, chukua tui weka sukari na vanilla. Ni vizuri tui liwe la uvuguvugu. Koroga mpaka sukari iyeyuke.

Weka kwenye unga, endelea kukanda. Kanda mpaka uone ukinyanyua unga kwa vidole, unanyanyuka wote haubaki kwenye sufuria.

Unga wa ngano ukiwa tayari umetengenezwa mabonge. Picha/ Margaret Maina

Mwagia mafuta ya uvuguvugu juu ya unga uliokanda huku ukiendelea kukanda mpaka mafuta yasionekane kwenye unga.

Funika kwa dakika tano uumuke, kisha anza kusukuma na kukata. Kata staili unayopenda.

Vipande vya unga wa ngano uliotayarishwa kabla kutumbukizwa kwa mafuta. Picha/ Margaret Maina

Bandika karai au sufuria yenye mafuta mekoni. Yakipata moto tumbukiza vipande vya mandazi – ule unga uliokatwakatwa -vianze kuiva.

Mandazi yakigeuka rangi na kuwa kahawia geuza upande wa pili.

Ukiona yameiva epua na ufurahie.