Makala

MAPISHI: Matoke na nyama ya ng'ombe

April 3rd, 2019 1 min read

Na MARY WANGARI

ULAJI wa ndizi umekuwapo Afrika tangu jadi.

Iwapo kuna mlo ambao hautakufeli wakati wowote basi ni mlo wa ndizi almaarufu kama matoke nchini Kenya.

Kando na kwamba ndizi ni chakula kinachosheheni afya tele, zinapatikana kirahisi na tena kwa bei nafuu.

Leo hii tutajifunza jinsi ya kuandaa mlo wa ndizi kwa nyama au ukipenda matoke ya nyama kwa njia rahisi ambayo kila na shekhe na yakhe anaweza kuimudu.

Waandalie jamaa na marafiki zako mlo huu na hakika utaridhishwa na matokeo yake.

(Mlo huu unaweza kuwatosheleza watu 4)

Viungo:

Vipande 10 ndizi mbichi

1 kilo Nyama

1 kopo la nazi

1 kijiko cha chumvi

1 ndimu

1 kijiko bizari ya manjano

3 Pili pili mbichi

2 nyanya kubwa

1 Kitunguu maji

1 kijiko Kitunguu saumu (thomu) na Tangawizi iliyosagwa

Maandalizi

  1. Kata nyama vipande vipande na uisafishe.
  2. Chemsha nyama, ongeza chumvi, thomu, tangawizi na ndimu. Iache itokote hadi iive.
  3. Kata kata nyanya na kitunguu, kisha mimina kwenye nyama inayochemka
  4. Ongezana bizari nusu kijiko. Wacha supu iive hadi ifanye rojo nzito weka pembeni. (supu iwe ya wastan, isiwe nyingi kupita kiasi).
  5. Menya maganda ndizi  na uzikate vipande vipande ukunwa wa wastan.
  6. Zioshe ndizi na uzitie ndani ya sufuria.
  7. Weka maji ndani ya sufuria kisha zichemshe ndizi mpaka ziwe laini kidogo.
  8. Mwaga maji ya ndizi kisha mimina supu na nyama ndani ya ndizi.

Mimina nazi, pilipili na bizari nusu kijiko ndani ya ndizi na uziweke kwenye meko zichemke mpaka zibakie na rojo kiasi. Onja chumvi na uongeze kadri utakavyopenda.

Weka pembeni zipoe.

Pakua mchuzi wa matoke ya nyama kwenye sahani au bakuli tayari kwa kuliwa. Unaweza kuambatisha na wali ukipenda kwa starehe yako!

 

Baruapepe ya mwandishi:  [email protected]