Makala

MAPISHI NA LISHE: Jinsi ya kupika uyoga na faida za kula chakula hiki

January 30th, 2020 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MOJAWAPO ya vyakula muhimu sana katika mwili wa binadamu vinavyoupa mwili nguvu na virutubisho vingi vya kujenga mwili ni pamoja na chakula kijulikanacho kwa jina la uyoga.

Uyoga ni kati ya vyakula vichache sana ambavyo vinaweza kukidhi mahitaji yote ya protini mwilini.

Uyoga pia una vitamini mbalimbali kama A, B, C, D, E, na K.

Una madini muhimu kama chuma, potashiamu, sodiumu, na fosforasi ambayo ni muhimu katika kujenga, kulinda afya na kudhibiti mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Madini mengine ni Zinki inayoimarisha kinga, Shaba inayosaida na Chuma kutengeneza chembechembe nyekundu za damu.

Kwenye uyoga kuna viini-lishe vinavyosaidia kuboresha mifumo ya mishipa ya damu, kuboresha mfumo wa kinga mwilini, na kukabiliana na maambukizi mwilini.

Vilevile Vitamini B iliyoko kwenye uyoga inasifika kwa uwezo wake wa kuzuia uchovu wa mwili (fatique) na akili hasa wakati wa kazi nyingi.

Vitamini B3 husaidia kupunguza kiwango cha mafuta mabaya ya Kolestroli mwilini, wakati Vitamini B6 yenyewe huondoa hatari ya mtu kukumbwa na kiharusi au moyo kusimama ghafla (Heart Attack).

Jinsi ya kuandaa

Muda wa kuandaa: Dakika 10

Muda wa kupika: Dakika 0

Walaji: 4

Vinavyohitajika

  • kilo 1 ya uyoga
  • siagi vijiko 2
  • kitunguu maji 2 (vikatekate)
  • nyanya ilosagwa vijiko 3
  • kitunguu saumu kijiko 1
  • pilipili manga ya unga ½ kijiko
  • oregano – 1 kijiko cha chai
  • parsely kavu iliyosagwa – 1 kijiko cha chai
  • mafuta ya kupikia
  • chumvi

Maelekezo

Osha uyoga vizuri kisha weka siagi katika sufuria ishike moto. Tia uyoga ukaange kidogo ili ulainike.

Katika sufuria ndogo, weka mafuta, kaanga kitunguu hadi vigeuke rangi.

Kisha tia nyanya na bizari zote halafu kaanga tena kidogo.

Ongeza uyoga katika ule mchanganyiko na ukaange kwenye moto wa wastani kwa dakika 20.

Epua ukiwa tayari na upakue na chochote ukipendacho.