Makala

MAPISHI: Ugali na sukumawiki

April 2nd, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

UGALI

Muda wa kusonga sima: dakika 15

Walaji: 2

Vinavyohitajika

–          Unga wa mahindi nusu kilo

–          Maji lita 1

Maelekezo

Mimina maji kwenye sufuria kisha bandika kwenye meko ili yachemke.

Tengeneza mchanganyiko kwa kuongeza unga kiasi kwenye maji yanayochemka huku ukikoroga.

Ongeza unga ukikoroga kwa mwiko hadi uwe mgumu.

Endelea kukoroga ukihakikisha hakuna mabonge ya unga hadi ugali uwe laini.

Punguza moto kisha funika ugali kwa dakika 10.

Epua na upakue.

 

Sukumawiki

 Muda wa kupika: Dakika 5

Walaji: 2

Vinavyohitajika

–          Sukumawiki

–          Pilipili kijiko 1

–          Chumvi kijiko 1

–          Maziwa vijiko 4

–          Kitunguu

–          Pilipili mboga

–          Mafuta ya kupikia

–          Kitunguu saumu kijiko 1

Sukumawiki zikiwa zimepikwa. Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Andaa kitunguu na pilipili mboga kwa kukata vipande vidogovidogo.

Andaa sukumawiki.

Bandika sufuria mekoni hadi ipate moto. Weka mafuta kisha weka sukumawiki. Koroga vizuri kisha funika na uache kwa dakika moja kisha koroga na uepue.

Kwenye sufuria nyingine, weka mafuta kisha kitunguu maji. Koroga, weka kitunguu saumu, pilipili na chumvi. Endelea kupinduapindua.

Weka pilipili mboga, koroga na uache kwa dakika mbili vichemke pamoja.

Weka sukumawiki, koroga vizuri kisha weka maziwa na uache ichemke kwa dakika 3 kisha epua.

Pakua na ugali na ufurahie.