Makala

MAPISHI: Wali wa nazi na nyama iliyosagwa

March 19th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MUDA wa kuandaa: Dakika 10

Mapishi: Dakika 30

Walaji: 4

Vinavyohitajika kwa ajili ya mapishi ya wali

 • Mchele nusu kilo
 • Tui la nazi kikombe 1
 • Maji lita (katika mapishi haya, maji ni mara mbili ya mchele. Hata hivyo, kuna wanaotumia mgao wa 1:3)
 • Chumvi nusu kijiko

Maelekezo

Osha mchele.

Weka mchele kwa sufuria ya upishi na ongeza chumvi. Acha mchele hadi uanze kuchemka katika sufuria iliyo mekoni.

Ukishaanza kuchemka, ongeza tui la nazi. Usikoroge.

Acha mchanganyiko uive taratibu kwa dakika 10.

Punguza moto na uache iive hadi maji yakauke.

Epua.

Vinavyohitajika kwa ajili ya kupika nyama iliyosagwa

 • Kima kilo 1
 • Vitunguu maji 2
 • Vitunguu saumu 2
 • Tangawizi 1
 • Nyanya 4
 • Mafuta ya kupikia
 • Chumvi kijiko 1
 • Karoti 2
 • Pilipili mboga 1
 • Juisi ya limau
Nyama iliyosagwa kabla ya kupikwa. Picha/ Margaret Maina

 

Maelekezo

Menya vitunguu, karoti, pilipili mboga na ukate kwenye vipande vyembamba sana.

Menya nyanya na tangawizi kisha katakata kwa kuchanganya pamoja.

Twanga vitunguu saumu kisha bandika sufuria ya kupikia mekoni.

Weka nyama na anza kukoroga ili kuzuia isigandie kwenye sufuria na kuungua huku ikifanya weusi usiovutia hata kidogo.

Weka kitunguu maji huku ukiendelea kukoroga kwa muda wa dakika 10.

Ongeza kitunguu saumu na tangawizi huku ukikoroga.

Weka mafuta ya kupikia kisha weka pilipili mboga, karoti na juisi ya limau. Ongeza chumvi kidogo. Endelea kukoroga.

Weka nyanya, koroga na funika sufuria uache kwa dakika 10.

Tazama baadhi ya picha za chakula hiki:

Wali. Picha/ Margaret Maina
Wali na nyama ya kusagwa. Picha/ Margaret Maina

Pakua na wali wa nazi na ufurahie pamoja na aila yako au marafiki.