Makala

MAPITIO YA TUNGO: Asali Chungu; Riwaya inayoangazia athari ya mazingira katika ulezi

July 17th, 2019 2 min read

Jina la utungo: Asali Chungu

Mwandishi: Said A. Mohamed

Mchapishaji: East African Educational Publishers Ltd

Mhakiki: Nyariki Nyariki

Kitabu: Riwaya

Kurasa: 213

ASALI Chungu imesheheni maudhui yanayozimulika jamii za sasa.

Athari ya mazingira katika ulezi wa watoto ni mojawapo ya maudhui yanayojitokeza wazi.

Semeni, msichana mbichi, mjakazi katika maskani ya Zuberi analikataa ombi la mapenzi la Bwana Zuberi. Bwana Zuberi anatumia hila kuhakikisha kwamba ‘ameikidhi’ tamaa yake.

Anamteka nyara Semeni kutoka kibandani pake kisha anambaka.

Baadaye, Semeni anajifungua mtoto wa kiume anayemwita Dude.

Dude anazaliwa na kukulia katika vibanda vya mbavu za mbwa ambapo Semeni na shoga yake, Bi Pili, wanaishi maisha ya kujichuuza kwa wanaume. Dude na Baya, bintiye Bi Pili, wanaanza kuiga tabia za wazazi wao wanapoachwa peke yao kibandani.

Baada ya kifo cha Semeni, Dude anajikuta jijini akitamba na ulimwengu mgumu. Ulevi na wanawake vinakuwa ibada kwake. Sadfa inamkutanisha na Bi Amina, mkewe Bwana Zuberi, ambaye anamtaka Dude kimapenzi. Dude anaikamia fursa hiyo kwa pupa na papara na kujipata akichovya asali ya yule anayepaswa kumwita ‘mama’.

Kukutana kwa Dude na Baya wakati Bi Amina na Dude wanatoka mandarini kunalitia doa penzi la Dude na Bi Amina. Amina anamvua Dude mamlaka na kumfurusha kwenye maskani ya kifahari aliyokuwa amemtengea.

Sadfa inapowakutanisha tena Bi Amina na Dude kupitia kwa Shemsa, binti ya Bi Amina na Bwana Zuberi. Dude analeta posa kwa wazazi wa Shemsa. Bwana Zuberi ambaye hana habari kuwa Dude ni mtoto wake aliyezaliwa na msichana aliyemvurugia maisha, anaikubali posa.

Bi Amina, ambaye dhamiri yake inamhukumu kutokana na uhusiano wake na Dude anaipinga posa yenyewe. Anamhonga Dude ili auvunjilie mbali uhusiano wake na bintiye bila mafanikio.

Ndoa

Hatimaye, Dude na Shemsa wanaoana.

Shemsa anajifungua mtoto wa kike anayemlanda sana Semeni. Dude anapendekeza mtoto aitwe Semeni.

Kutajwa kwa jina Semeni kunamfanya Bwana Zuberi kung’amua kuwa Dude ni mwanawe. Huo unakuwa mwanzo wa masaibu yanayoanza kumwandama Zuberi.

Dude amevuka mipaka kwa kumringa Latifa, dadaye Shemsa. Zuberi anapata mnong’ono kuwa Dude amewahi kuwa mpenzi wa pembeni wa ‘mama yake’.

Chanzo cha Masaibu yanayowaandama Dude na Bwana Zuberi ni tamaa ya Zuberi mwenyewe na mazingira ya ulezi wa Dude.

Mvuto wa Asali Chungu umechangiwa na matumizi ya kiufundi ya taharuki baada ya taharuki. Lugha imetononoshwa kwa matumizi ya tamathali mbalimbali za usemi.