Makala

MAPITIO YA TUNGO: Kangaruu wa Samawati; Hadithi inayopigia chapuo haja ya kutambua vipawa

March 13th, 2019 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

Jina la utungo: Kangaruu wa Samawati
Mwandishi: Bitugi Matundura
Mchapishaji: Queenex Publishers Limited
Mhakiki: Nyariki E. Nyariki
Kitabu: Hadithi ya watoto
Kurasa: 38

LICHA ya kazi za kutwa darasani, watoto wana mahitaji mengine ya msingi ambayo wazazi, walimu na wadau wengine wa elimu wanapaswa kuyatambua na kuyakidhi kama njia moja ya kuwafanya kujithamini maishani.

Kwa mfano, baadhi ya watoto wametunukiwa vipawa mbalimbali ambavyo vinapaswa kutambuliwa mapema katika maisha yao, kuchochewa na kupaliliwa.

Katika simulizi hii, mwandishi Matundura anakiangazia kipawa kimojawapo.

Matendechere anagundua kuwa ana kipawa cha uigizaji akiwa katika darasa la tatu.

Mwalimu wa darasa na wazazi wa Matendechere wanamtilia upondo katika kuitimiza ndoto yake ya uigizaji.

Jambo hilo linampa motisha sana na kuzizima fikra za uonevu alizokuwa ameanza kuzitendekeza tangu utotoni.

Wakoli, kaka yake Matendechere, anaonekana kuvuta kimo kwa kasi.

Katika hali hiyo, Matendechere anafaidi mavulia ya Wakoli wakati ambapo Wakoli anafaidi mavazi mapya.

Jambo hili linamfanya Matendechere ambaye alitaka kununuliwa mavazi mapya kuanza kuwa na hisia za uchukivu.

Jambo jingine ambalo linamfanya kuhisi kwamba ameonewa ni pale anapotengwa katika michezo yote ambayo Wakoli na masahibu wake wanashiriki kwa kisingizio kwamba bado alikuwa angali mdogo.

Hata pale ambapo Matendechere anajaribu kucheza na mnuna wake, Sabina, Sabina anaonekana kutofikia kiwango chake cha uchezaji hivyo basi wanaishia kuzozana kila wakati.

Mabadiliko makubwa yanajiri katika maisha ya Matendechere anapogundua kwamba anaweza kuigiza.

Kupitia kwa mwalimu wake wa darasa, Matendechere anaomba kushirikishwa katika mchezo huo wa kuigiza ambao uliwahusisha wanafunzi wa darasa la sita.

Mwalimu wa drama, Bi Sperantia, anapomruhusu Matendechere kuigiza sehemu ya ‘Kangaruu wa Samawati’ katika mchezo huo, moyo wa Matendechere unabubujikwa na furaha.

Wazazi wake nao wako radhi kuenda kumtazama mwana wao akiuigiza mchezo huo ukumbini.

Bi Sperantia anamchochea na kumshajiisha Matendechere kuiigiza sehemu yake vyema.

Mwishoni mwa mchezo, Matendechere anapokea sifa kochokocho kutoka kwa Bi Sperantia.

Jambo hili linamfanya aanze kujithamini maishani na kususia hisia za chuki alizokuwa nazo dhidi ya umbu zake.

Baadhi ya vipawa vya watoto vinapotambuliwa mapema vinaweza kuwa njia mojawapo ya watoto hao kujipatia “mchumo” katika maisha yao ya baadaye.

Bwana Matundura ameitumia lugha nyepesi na tononofu katika kuisuka hadithi hii. Kazi hii inawaafiki zaidi wanafunzi wa darasa la nne, tano na sita.